BAADA YA WAARABU KUWAFUNGA YANGA, CHIRWA SASA KUKIONA CHA MOTO




Kutokana na sakata la mshambuliaji wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa kugomea kujiunga na wenzake kwenda Algeria katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya nchini humo, straika huyo anaweza kukumbana na balaa.

Chirwa aligoma kusafiri na timu akidai anasubiri hadi alipwe mishahara yake ya miezi mitatu, matokeo yake Yanga ilikumbana na kipigo cha mabao 4-0 juzi na kutolewa na Waarabu hao katika michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.  

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi, amesema kuwa mara baada ya wachezaji wote kurudi, watamweka kiti moto Chirwa na watatangaza hadharani azimio lao juu yake.

Siku moja kabla Yanga haijaenda Algeria, Chirwa aligoma kuungana na wenzake kwa madai kwamba hajalipwa mishahara yake ya miezi mitatu.

Mkemi alisema kuwa suala la Chirwa kutoungana na wenzake katika msafara ulioenda Algeria, wanatarajia kuliongelea hivi karibuni baada ya timu kurejea nchini, kisha watalitolea ufafanuzi.

“Kweli Chirwa hajaungana na wenzake na suala la mishahara inayodaiwa mimi najua tayari wameshapewa, hivyo tutakaa naye baada ya timu kurudi kisha tutalitolea ufafanuzi wake mara moja baada tu ya kikosi chetu kurejea kutoka Algeria.


“Naomba wapenzi na mashabiki wetu wawe na subira, siku si nyingi watapata ufafanuzi sahihi wa jambo hilo,” alisema.

SOURCE: CHAMPIONI
Powered by Blogger.