WAZIRI MAKAMBA AENDELEA KUNG'AMUA CHANGAMOTO ZA KIMAZINGIRA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akimsikiliza Bw. Richard Kuyangana akiwasilisha maoni ya wananchi wa Hale katika Mkutano wa Hadhara. Waziri Makamba amewataka wananchi hao kutii sheria, kanuni na taratibu za hifadhi ya mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akipanda mti aina ya 'Mnyasa' katika kuunga mkono kampeni endelevu ya upandaji miti nchini, katika Msitu wa Amani.
Faida ya Hifadhi endelevu ya Mazingira. Pichani ni kibanda maalumu kwa ajili ufugaji wa vipepeo katika Kijiji cha Fanusi Wilayani Muheza. Wananchi wa eneo hilo wamekua wakinufaika na uuzwaji wa vipepeo hao nje ya chini na kuboresha hali zao za maisha.
Na Lulu Mussa
Ziara maalumu ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. January Makamba kutembelea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania yenye lengo la kung’amua changamoto za kimazingira, athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo, imeingi siku ya nne.
Hii leo Waziri Makamba ametembelea Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, na kupokea taarifa ya hali ya Mazingira Wilayani hapo taarifa iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi MwanaAsha Tumbo.
Bi Tumbo ameainisha changamoto za kimazingira katika Wilaya yake kuwa ni pamoja na kuwa ni pamoja na Uvuvi haramu, Mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na shughuli za binadamu zisizozingatia uhifadhi endelevu ya mazingira ikiwa ni pamoja na ukataji ovyo wa miti ya asili na misitu ya kupanda, kilimo cha kuhamahama na uchimbaji wa madini katika kingo na pembezoni mwa vyanzo vya maji.
Bi. Tumbo amesema kuwa hivi sasa wilaya ya Muheza inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mvua kutoka misimu mitatu kwa mwaka hadi kufikia msimu mmoja tu. "katika siku za hivi karibuni kumekua na ongezeko kubwa la uchimbaji holela wa madini unaopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira". Ili kuimarisha doria kikamilifu wakazi wa Wilaya ya Muheza wamewasilisha ombi maalumu la kujengewa nyumba za askari hii ni baada ya kupata msaada kutoka United Nations Development Programme ambao wamekubali kujenga kituo cha polisi.
Aidha, jitihada mbalimbali zimechukuliwa na uongozi wa Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka zuio la ukataji miti hovyo. Miti iliyopigwa marufuku ni pamoja na miti iliyooteshwa kwa juhudi za watu binafsi na hata ile ya mashirika/taasisi. 
Kwa upande wake Waziri Makamba  ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa juhudi za dhati za kuhifadhi mazingira, pia kuanzishwa kwa kampeni maalumu ya kupanda miti. Jitihada nyingine ni pamoja na kufukia mashimo yote yaliyochimbwa na wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Kihara, katika msitu wa Amani.
Katika siku hii ya nne Waziri Makamba alipata fursa ya kutembelea "Amani Nature Researve" ambapo alishuhudia ni kwajinsi gani mazingira yamehifadhiwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa mradi wa kuzalisha vipepeo na kuuza nje ya nchi biashara ambayo imekua ikiwasaidia wakazi wa kijiji hicho katika kusomesha watoto wao na kujenga nyumba bora za kuishi.
Wakazi hao wa kijiji cha Kata ya Fanusi walianisha changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa kuwa ni kukosa soko la kuuza vipepeo hao baada ya kuzuiwa na Serikali. "Niwahikikishieni kuwa suala hili tutalichukua na kulifikisha katika Wizara husika na naamini litafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo" Makamba alisisitiza.
Nae Mhifadhi wa msitu wa Amani Bi.Mwanaidi Kijazi ameainisha umuhimu huo  kuwa ni pamoja na hifadhi ya bionuai na mifumo ya ikojia, hifadhi ya viumbe hai adimu duniani, maumbile ya asili maalumu kwa utunzaji wa vinasaba na chanzo kikubwa cha vyanzo vya maji.
Ziara ya Waziri Makamba katika mkoa wa Tanga  hii leo imefanyika katika Wilaya ya Muheza ambapo ameshiriki katika zoezi la kupanda miti, kutembelea misitu wa Amani na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kihara na kuwasisitiza wakazi wa eneo hilo kutunza rasilimali zilizopo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, katika kuchangia shughuli za maendeleo kijijini hapo Waziri Makamba ameahidi kununua miche ya miti 150,000 kwa ajili ya kuigawa maeno mbalimbali ya wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada kwa wakazi hao kupanda miti kwa wingi kwa lengo la kulinda na kutunza mazingira.
Powered by Blogger.