Serikali Yaendelea Kuboresha Uwekezaji Katika Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo Ndogo
|
Katibu
Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm
Meru akifungua warsha ya siku moja ya tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda
Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
|
|
Katibu
Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm
Meru (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Viwanda Vidogo na
Biashara Ndogo Bw. Boniface Michael.
|
Picha
na: Frank Mvungi
Na
Fatma Salum
Serikali
kupitia Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji inaendelea kufanya maboresho
ya sekta ya viwanda ili kuendana na kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda
hapa nchini.
Hayo
yamebainishwa na Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na
Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru wakati akifungua warsha ya siku moja ya tathmini
ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika leo Jijini
Dar es Salaam.
Dkt.
Meru alieleza kuwa lengo la kufanya tathmini hiyo ni kuboresha mazingira ya
uwekezaji kwenye viwanda vidogo na vya kati kwa kuwa kuna mabadiliko mengi
yamefanyika tangu sera hiyo ianze kutumika mwaka 2003.
“Viwanda
hivyo vinachangia asilimia 27 ya pato la taifa hivyo ni muhimu kupitia upya
sera hii na kupata maoni ya wadau kwani hivi sasa kuna mabadiliko mengi ya
teknolojia, sheria na taratibu za uwekezaji.” Alisisitiza Dkt. Meru.
Aidha
alisema kuwa Serikali itafungua dirisha dogo kwenye Benki ya Uwekezaji (TIB)
kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji wa viwanda vidogo na vya kati kupata mitaji
ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao.
Akieleza
mipango ya baadae Dkt. Meru alibainisha kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha
Benki ya Maendeleo ya Viwanda itakayowawezesha wazawa na wawekezaji wengine
kupata mitaji yenye riba na masharti nafuu ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.
Dkt.
Meru alitoa wito kwa Watanzania kujikita kwenye uwekezaji wa viwanda kwa kuwa
ndio njia pekee ya kukuza uchumi kwa haraka na kuongeza ajira, teknolojia,
biashara na mitaji.
Tathmini
ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda imekusudiwa kutoa mwelekeo wa namna bora ya
kujikita kwenye uchumi wa viwanda kupitia uwekezaji wa viwanda vidogo na vya
kati.