Baadhi ya Maafisa
Waandamizi wa Serikali wanaohusika na elimu kutoka nchi sita za Afrika
wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia (hayupo pichani), Venance Manori wakati wa
ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha maafisa hao katika kutengeneza mipango
inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu.Warsha hiyo ya siku tatu
imefunguliwa jana jijini Dar es Salaam.
Na
Jacquiline Mrisho.
Serikali
imejipanga kutengeneza mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata
mimba wakiwa masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi kufikia ngazi za juu.
Hayo
yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka
kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori alipokuwa akifungua
warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika
katika kutengeneza mipango inayozingatia jinsia katika elimu kwa niaba ya
Waziri wa Wizara hiyo Prof. Joyce Ndalichako.
Manori
amesema Serikali ya Tanzania inajitahidi kuzingatia jinsia katika utoaji wa
elimu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya Msingi na Sekondari uwiano wake ni
moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana hupungua kutokana na changamoto
mbalimbali zinazowakumba hivyo lengo la warsha hiyo ni kuwasaidia wadau kuweka
mipango ya elimu inayozingatia usawa wa kijinsia.
“Serikali
yetu imejipanga kuhakikisha wasichana wanapata elimu hadi ngazi za juu lakini
mpango huo unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba na ndoa za
utotoni hivyo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ngazi za juu za elimu tuko
kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo kwa ajili ya wanafunzi waliopata mimba
wakiwa bado wanasoma kupata nafasi ya kuendelea na masomo,”alisema Manori.
Mkurugenzi
Msaidizi amezitaja changamoto zingine zinazowapelekea wanafunzi wa kike kuacha
shule zikiwemo za umaskini, mazingira rafiki ya kusomea, mila na desturi
zinazomkataza msichana kupata nafasi ya kusoma pamoja na kukosa muda wa
kujisomea kwa sababu ya kufanya kazi nyingi wanaporudi majumbani.
Manori
ametoa rai kwa Watanzania kuelewa kuwa kila mtoto ana haki na wajibu wa kupata
elimu bila kujali jinsia pia ameiasa jamii kuacha kuwaozesha wasichana wenye
umri chini ya miaka 18 ili waweze kufikia malengo yao waliyojipangia.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen
Haldorsen ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha
mipango ya elimu nchini inaangalia usawa wa kijinsia kwa kuwa ni njia moja wapo
itakayochochea maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.
“Warsha
hii imeandaliwa kwa ajili ya wadau wote kutoa mawazo yao juu ya changamoto za
usawa wa kijinsia zinazoikumba sekta ya elimu pamoja na kuwapa fursa wadau hao
kushauriana kuhusu mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo ili kuinua
sekta ya elimu sio tu kwa Tanzania bali kwa Afrika nzima,”alisema Haldorsen.
Haldorsen
ameongeza kuwa mfumo wa elimu umetambua uhusiano uliopo kati ya elimu na usawa
wa kijinsia ndio maana wadau wa masuala ya elimu wa Serikali kutoka katika
baadhi ya nchi za Afrika wameamua kuungana kwa pamoja kujadili juu ya tathmini,
mpangilio na ufuatiliaji wa elimu unayozingatia jinsia.
Tanzania
imekua nchi ya kwanza kuendesha warsha hiyo ya siku tatu iliyoshirikisha
maafisa waandamizi wa Serikali wanaoshughulikia mipango ya elimu kutoka nchi za
Mozambique, Zambia, Malawi, Uganda, Zanzibar na Tanzania Bara.
Imeandaliwa
kwa ushirikiano wa shirika la Plan International- Tanzania, Global Partnership
for Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations Girls’ Education
Initiative (UNGEI).
|