Waziri Lukuvi Apiga Marufuku Wathamini Wanaofanya Uthamini Nje Ya Serikali
Waziri
wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi leo amezindua
rasmi bodi ya wathamini ambayo imeundwa kwa mujibu wa sheria ya uthamini
na usajili wa wathamini ya mwaka 2016 ambayo imeanza kutumika rasmi
Januari mwaka huu.
Akizungumza
katika uzinduzi huo Waziri Lukuvi amesema kwa mujibu wa sheria wajumbe
wa bodi ni lazima kutoka katika taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya
ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, ofisi ya Rais TAMISEMI, vyuo
vikuu, vyama vya kitaluma vya wathamini, ofisi ya mwanasheria mkuu,
taasisi ya mabenki, na bodi ya wakaguzi na wahasibu(NBAA) na kuongeza
kuwa kwa muundo huo bodi inahitaji mpana mkubwa wa uwakilishi ili
kutekeleza majukumu yake kwa urahisi.
Pia
amesema kuwa serikali iliona umuhimu wa kuwa na chombo madhubuti kwa
ajili ya kusimamia taaluma ya uthamini baada ya kuonekana kuwa kumekuwa
na ongezeko la udanganyifu katika kazi ya uthamini hasa kwenye miradi ya
serikali na ya mikopo katika mabenki baada ya Kazi hiyo ya uthamini
kuwa chini ya Baraza la wapima ardhi na wathamini (NCPS).
Aidha
ameweka wazi kwamba tasnia ya uthamini ni ya muhimu sana kwa ustawi wa
uchumi kwa ujumla kwani Kazi za wathamini zunahusiana na ukadiriaji wa
Mali kwa malengo mbalimbali ikiwemo kuweka rehani za mikopo kwenye
mabenki, kodi za ardhi na majengo, mahesabu ya makampuni binafsi na
taasisi za serikali hivyo kama Kazi hiyo haitafanywa kwa umakimi na
uadilifu inaweza kuchangia kuanguka kwa uchumi na hata watu kupoteza
mali sambamba na kusababisha migogoro ya ardhi.
Pia
amebainisha masuala ambayo yanatakiwa kufanyiwa Kazi kwa haraka ili
kufuta dosari zilizopo na kusema kuwa ni kudhibiti kazi ya uthamini
kufanywa na watu wasiosajiliwa na bodi na wale wasio ma taaluma ya
uthamini, kudhibiti udanganyifu wa thamani kwa ajili ya uthamini kwa
ajili ya fidia, kodi na mikopo ya benki, kutoa na kusimamia mafunzo ya
Mara kwa Mara kwa wathamini pamoja na kuandaa viwango na miongozo ya
uthamini.
Pia
Waziri ametoa onyo kwa wathamini wanaotumia udanganyifu pindi
wanapofanya tathimini pamoja na wale wanaofanya kazi ya uthamini nje ya
kazi au miradi ya serikali na kuwaomba wathamini wote kujisajili kwenye
bodi ya wathamini ili watambulike na kupata usajili unaotambulika.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa bodi ya usajili wa wathamini Dkt.Cletus
E.Ndjovu amesema kuwa bodi ya wathamini ni muhimu sana katika suala la
maendeleo na kuahidi kwamba watafanya kazi kwa weledi na kwa kufuata
sheria ya bodi ya uthamini bila kumwonea mtu aibu ili kuleta heshima
katika taaluma ya uthamini.
