Waziri Mkuu Azindua Mpango Mkakati Wa Afya Moja
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Mpango Mkakati wa Afya Moja na Dawati la
Kuratibu Afya Moja nchini ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania
inaendelea kuwa mahala safi na salama kwa kuishi na kufanya kazi za
kimaendeleo.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati akizindua mpango
mkakati huo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo
amesema dhana ya Afya Moja inafaa kutumika zaidi katika nchi
zinazoendelea.
Waziri
Mkuu amesema mbali na mpango kufaa kutumika katika nchi zinazoendelea
pia hata kwa nchi zinazokaribia maeneo ya wanyama pori kama Tanzania
kutokana na kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali.
Amesema
kwa upande wa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuwa Bara
hilo, lina sehemu nyingi zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama kama
Bonde la Mto Kongo, ambalo mazingira yake yamekuwa ni kitovu cha
magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa (RVF), Marburg
na mengineyo.
Waziri
Mkuu amesema kwa kutambua hilo, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la
Maendeleo la Marekani (USAID) na wadau wengine wa Maendeleo, imeendelea
kutekeleza agenda ya Afya Moja nchini tangu mwaka 2013 ilipozinduliwa
kwa mara ya kwanza mjini Arusha na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohamed
Gharib Bilal.
“Utekelezaji
wa Mpango huu unakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi (2015-2020) ya kujenga Taifa lenye watu wenye afya
bora itakayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali ambayo
ni muhimu sana katika kufikia azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa
Viwanda.”
Awali,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na
Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama alisema uzinduzi wa mkakati huo ni
ngao tosha kwa nchi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa.
Alisema
pamoja na kutekeleza kanuni za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ambazo
zinahitaji ushirikiano wa sekta mbalilmbali kwa kutumia dhana ya afya
moja, mpango mkakati huo unaleta msukumo katika Ofisi ya Waziri Mkuu
kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali kudhibiti magonjwa.
Bibi
Jenista alisema uratibu wa afya moja unakwenda sambamba na matakwa ya
Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya
Wanyama (IOE) na Shirika la Kimataifa la Chakula la Kilimo (FAO) ambayo
yanashirikiana katika kudhibiti magonjwa yanayoambukiza na usugu wa
dawa.
