Waziri Mkuu: Bahari Kuu, Viwanja Vya Ndege Vyabainika Kupitisha Dawa Za Kulevya
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini kwamba maeneo ya bahari
kuu, bandari, vituo vya mabasi na viwanja vya ndege yanayotumika sana
katika kupitisha dawa za kulevya.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amesema wafanyabiashara, wasambazaji na watumiaji wa
dawa za kulevya wameendelea kukamatwa, lengo ni kuhakikisha biashara
hiyo inamalizika nchini.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati
akikabidhi gari kwa Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Siyanga kwenye viwanja vya
Karimjee jijini Dar es Salaam.
Amesema
mbali na kukamata meli, pia Serikali imewakamata wasambazaji pamoja na
kundi kubwa la wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za
kulevya sambamba na watumiaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa
salama na kizazi chenye uwezo wa kuzalisha mali.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za
kulenya, ambapo hivi karibuni imekamata meli nyingi, moja ilikiwa
inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya Mtwara ikiwa na dawa
nyingi za kulevya.
“Niwakati
wa Serikali kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na
Dawa za Kulevya na leo hii tunawakabidhi gari hili jipya kabisa ili
iweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo.”
Pia
Waziri Mkuu amewataka Watanzania waachane na biashara ya dawa za
kulevya ikiwa ni pamoja na kazi ya kusambaza, kuzalisha na kutumia na
watakaokamatwa wakijihusisha nayo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema
kwa sasa Serikali inajenga maabara ambayo itatumiwa na Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kufanya uchunguzi
wa dawa wanazozikamata.
Waziri
Mkuu amesema wananchi wanatakiwa kushirikiana na Serikali katika vita
dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa mara wanapowabaini
wafanyabiashara, watumiaji na wasambazaji wa dawa hizo. Pia wahakikishe
wanawalinda vijana ili wasijihusishe na dawa za kulevya.
Kwa
upande wake Siyanga aliishukuru Serikali kwa kuipatia mamlaka hiyo
gari, ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waachane na biashara
ya dawa za kulevya. Alisema wanapambana kuhakikisha dawa za kulevya ili
zisiingie nchini.
Alisema
mbali na kudhibiti biashara hiyo, pia wanatoa elimu juu ya madhara ya
matumizi ya dawa za kulevya vikiwemo vitendo viovu vinavyofanywa na
watumiaji ili wachukie na waache kutumia dawa hizo.
Pia
wanafanya kazi ya kuwahudumia watu walioathirika na matumizi ya dawa za
kulevya, hivyo aliwaomba wananchi kutowanyanyapaa waathirika na badala
yake wawapeleke katika vituo maalumu vya kutolea huduma za methadone.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 13, 2018.
