WANAUME ARUSHA WAGOMA KWENDA KLINIKI NA WAKE ZAO
Kampeni ya kuwataka wanaume waongozane
na wenza wao wajawazito kiliniki kwa ajili ya kupata ushauri wa
kitaalamu kuhusu afya ya uzazi sambamba na uzazi wa mpango, inaelekea
kukwama katika jiji la Arusha na hivyo kutishia kinamama kukosa
matibabu.
Katika kampeni hiyo ambayo mama anayeshindwa kufika na mumewe kiliniki hunyimwa cheti ili kuweka mkazo suala hilo.
Kutokana na hali hiyo, suala hilo
limesababisha wajawazito jijini Arusha kubuni mbinu mpya ya kukodi
vijana kuwasindikiza hospitali.
Naibu Meya wa Jiji la Arusha ambaye pia
ni mwenyekiti wa kamati ya madiwani wa kupambana na Ukimwi, Viola
Likindikoki alitoa taarifa hiyo juzi wakati akiwasilisha taarifa yake ya
robo tatu ya mwaka uliomalizika Januari mwaka huu.
Amesema mgomo wa wanaume wengi katika
jiji la Arusha, unawapa wakati mgumu wanawake wanaotakiwa kuambatana
na waume zao kliniki kutokana na kuwakatalia hivyo kuwalazimu kukodi
vijana ili mradi tu waonekane na waume zao ili wapatiwe huduma.
Amewataka viongozi wote wa ngazi ya kata
na vijiji kuungana kusisitiza umuhimu wa watu wote kuhudhuria kliniki
au kupima maambukizo kwa lengo la kutambua hali halisi na kupata msaada
wa haraka.
“Unajua wafadhili waliokuwa wanafadhili
hizi kampeni za kutokomeza Ukimwi wengi wamejitoa, hivyo sisi viongozi
tunaowawakilisha wananchi tusibweteke bali iwe chachu ya sisi kupambania
maisha ya wananchi wetu.”
Akizungumza na waandishi wa habari,
Diwani wa Ngarenaro, Issaya Doita amesema wanaume wengi wanakimbia
kuongozana na wanawake hao kutokana na wengi siyo waume zao au wanabanwa
na shughuli nyingi za kikazi
“Huu mji ni wa utalii, una pilikapilika
nyingi za kusaka uchumi wa nyumbani hivyo wanaume wengi wanakwambia wana
kazi nyingi hawawezi kwenda kukaa kliniki halafu jioni walale njaa,
lakini sababu nyingine wanayotuambia baadhi yao si wake zao bali ni
‘mchepuko’ hivyo wanaogopa taarifa zao kuwekwa,” amesema Doita.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani
Kihamia amesema watahakikisha wanawake kliniki wanakuwa na waume zao la
sivyo watafuatilia taarifa zao na watakaobainika kukodi vijana
wataumbuliwa.
N a Bertha Ismail, Mwananchi