CHADEMA WASITISHA KAMPENI ZA UDIWANI MULEBA
Viongozi wa Chadema wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, wamesitisha shughuli
za kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa Buhangaza Mchungaji Nelson
Athanasio Makoti ili kupata nafasi ya kushughulikia matibabu yake baada
ya kuhamishwa Hospitali ya Kagondo hadi Dar es Salaam kwa matibabu.
Katibu mwenezi wa Chadema Muleba Kusini, Hamisi Yusufu amesema hawezi
kutaja alikolazwa mgombea huyo kwa sababu za kiusalama kutokana na hali
ya upepo ulivyo kisiasa hapa nchini.
Amesema kampeni za uchaguzi wa udiwani Kata ya Buhangaza, zitaendelea kesho.
"Suala la wapi mgombea amelazwa msemaji wake anaweza kuulizwa Tumaini
Makene lakini kwa taarifa nilizopokea asubuhi ya leo ameonyesha
mabadiliko tofauti na ilivyokuwa Kagondo," amesema Yusufu.
Hata hivyo, amesema wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu na kwa sasa
Chadema hawaelekezi tuhuma zozote kwa kundi lolote la kisiasa.
Amesema jukumu kubwa ni vyombo vya dola kufanya kazi ya kuchunguza na
kubaini waliohusika kwa kusababisha mgombea kuathirika kiafya.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Isack Msangi amesema katika
mahojiano na Makoti na ndugu zake na wananchi hakuna mtuhumiwa
anayeshikiliwa japo upelelezi unaendelea.
Msangi amesema saa tisa alasiri ya leo jeshi hilo litatoa ufafanuzi
kuhusu mwenendo wa kufuatilia tukio la mgombea huyo na mahali alipo ili
kuwaweka sawa wananchi wanaofuatilia kinachofanyika dhidi ya mpendwa
wao.
Na Shaaban Ndyamukama ,Mwananchi