SSRA, Nida kushirikiana uandikishaji vitambulisho vya Taifa
Mamlaka
ya Usimamizi wa Mifuko ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) wanaendelea na
awamu ya pili ya uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wanachama wa
mifuko yote ya hifadhi ya jamii.
Awamu hiyo itaanza Februari, 5 hadi 28, 2018 katika wilaya tano za Dar es Salaam.
Akizungumza
leo Februari2, 2018 meneja miradi wa SSRA, Sara Kibonde amesema lengo
la uandikishaji huo ni kuboresha taarifa za wanachama wa sekta ya mifuko
hiyo nchini.
Amesema
uandikishaji huo ulianzia mkoani Dodoma, ulikuwa ni mpango maalumu
lakini waligundua kuwa asilimia 51.2 ya wachangaji na wanufaika wa
mifuko hiyo hawana vitambulisho vya Taifa .
Amebainisha
kuwa mifuko hiyo ina wachangiaji zaidi ya milioni moja na wanufaika
zaidi ya milioni mbili, huku asilimia 48.8 pekee ndi wenye vitambulisho
vya Taifa.
“Tunashirikiana
na Nida kuhakikisha wachangiaji na wanufaika wa mifuko hii wote
wanakuwa na vitambulisho vya Taifa, ”amesema Kibonde.
Meneja
wa takwimu wa Nida, Francis Saliboko amesema wamejipanga ipasavyo
kuhakikisha wanamaliza changamoto zote zilizojitokeza awali katika
uandikishaji na utoaji vitambulisho hivyo.
“Hakuna
atakayepata namba mbili au vitambulisho viwili, kama alijiandikisha
mahali popote na tukachukua alama zake za vidole akiingiza taarifa
nyingine ataonekana,”amesema.