TAKUKURU yawatia mbaroni watu wanne kwa Rushwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Temeke imewakamata watu wanne, akiwemo ofisa mtendaji Kata ya Jangwani,  Emanuel Kobelo baada kujifanya maofisa kutoka ofisi ya Rais, kupokea rushwa ya Sh2milioni kutoka kwa mfanyabiashara wa madini.

Mkuu wa Takukuru mkoani humo, Pilly Mwakasege amewataja wengine waliokamatwa kuwa ni ofisa mstaafu wa Jeshi la Magereza, Joseph Chilumba ambaye alijitambulisha kama ofisa Usalama wa Taifa, mfanyabiashara wa kampuni ya Equalmalk, Ally Ally na Doroth Magige.

Amesema Januari 30, 2018 waliwawekea mtego watuhumiwa hao na kuwakamata baada ya kuomba rushwa ya Sh3milioni, kupokea Sh2milioni ili wasimchukulie hatua mfanyabiashara huyo  waliyemtuhumu kushirikiana na raia wa kigeni ambao wanafanya biashara ya madini ya dhahabu na almasi.

“Kutokana na kosa la kushawishi kuomba na kupokea rushwa watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo na kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007 katika mahakama ya wilaya ya Temeke,” amesema.

Mwakasege amewatahadhalisha watumishi wa umma na wananchi kutojihusisha na vitendo vya rushwa, atakayebainika atachukuliwa hatua bila kuonewa aibu.
Powered by Blogger.