Serikali Yafanikiwa Kurejesha Mali Za NCU, SHIRECU
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kurejesha mali tisa
kati ya 10 za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) ambazo
zilichukuliwa kinyume cha taratibu na kuagiza watuhumiwa wachukuliwe
hatua za kisheria.
Amesema
mali moja iliyobakia bado inafanyiwa uchunguzi na mali mbili za Chama
Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) nazo pia zimepatikana lakini
bado ziko kwenye hatua ya makabidhiano.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini
Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11.
Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
Waziri
Mkuu amezitaja mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU)
zilizorejeshwa kuwa jengo la Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd.
maarufu kwa jina la “Transport House” au KAUMA House, lililopo katika
kiwanja namba 242, Kitalu T, Mtaa wa Stesheni; kiwanda cha kusindika
mafuta cha New Era Oil Mill, kilichopo katika eneo la Igogo; na jengo na
viwanja vya Ashock Industries vilivyopo eneo la viwanda Igogo.
Nyingine
ni majengo ya kilichokuwa kiwanda cha mkonge na dengu kilichopo eneo la
Igogo kwenye kiwanja namba 41 na 79; jengo lililopo katika kiwanja
kilichopo Isamilo namba 80, kitalu “D”; jengo lililopo katika kiwanja
kilichopo Isamilo namba 110, kitalu “D” na ghala moja katika kiwanja
namba 104, kitalu “A” kilichopo eneo la Igogo.
“Mali
nyingine zilizorejeshwa ni jengo moja lililopo mjini Geita katika
kiwanja namba 8 Kitalu “K”; jengo moja lililopo mjini Geita, katika
kiwanja namba 24, Kitalu “K” na jengo lililopo Isamilo katika kiwanja
namba 89 Kitalu “D”,” amesema Waziri Mkuu.
Kwa
upande wa mali za SHIRECU, Waziri Mkuu amezitaja mali zilizopo kwenye
hatua ya makabidhiano kuwa ni ghala lililopo Kurasini, Dar es Salaam na
nyumba ya ghorofa tatu iliyopo kiwanja namba 1001 “BB” Ilala, jijini Dar
es Salaam.
“Katika
kusimamia misingi ya utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa vyama
vya ushirika, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi maalum kuhusu
mikataba mibovu ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama
Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha
Kagera (KCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).
Vilevile, tunachunguza kushikiliwa kwa mali za ushirika bila kufuata
utaratibu,” amesema.
Amesema
Serikali itaendelea kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na vyama
vikuu vilivyosinzia katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara na
kwamba juhudi na hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga
kuongeza imani, hamasa na uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake,
na hivyo, kuinua kipato cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya
kujiajiri wenyewe katika sekta ya kilimo.
