Waziri Mkuu: Viwanja Zaidi Ya 15,000 Vimepimwa Dodoma, Kuanza kuuzwa Machi 30, mwaka huu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Dodoma imekamilisha upimaji wa
viwanja vipya zaidi ya 15,000 na vitaanza kugawiwa Machi, 30 mwaka huu.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini
Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11.
Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
“Kutokana
na agizo la Serikali la kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, mahitaji
ya viwanja hadi Februari 2018 yalikuwa ni viwanja 24,602. Manispaa ya
Dodoma hivi sasa inatekeleza mkakati wake wa kuzalisha viwanja 30,000
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Tayari upimaji wa viwanja vipya
15,316 umekamilika na vitaanza kugawiwa kuanzia tarehe 30 Machi 2018,”
amesema Waziri Mkuu.
Amelieleza
Bunge kwamba kiasi kilichobaki cha viwanja 14,684 kitakamilika ifikapo
Juni, 2018 na wananchi watauziwa viwanja hivyo kwa bei elekezi
itakayotolewa na Manispaa hiyo.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi na watumishi wa umma
watakaohitaji viwanja kufuata taratibu za maombi ya viwanja pindi
vitakapotangazwa rasmi na kusisitiza kuwa zoezi la kubadilisha hati
zilizotolewa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
(CDA) na kupata hatimiliki za miaka 99 linaendelea. “Wenye hati za CDA
mnasisitizwa kuendelea na taratibu za kuzibadilisha,” amesema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema jumla ya watumishi 3,829 kutoka
wizara na taasisi mbalimbali za Serikali tayari wamehamia Dodoma akiwemo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan.
“Napenda
kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ofisi yake
walihamia rasmi Dodoma tarehe 15 Desemba, 2017 kama ilivyopangwa,”
amesema.
Kuhusu
mpango wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Waziri Mkuu amesema Serikali
imedhamiria kuifanya Dodoma iwe na ukanda wa kijani (Green Belt) kupitia
mpango wa kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya msitu wa
Mahomanyika wenye ukubwa wa hekta 2,000; msitu wa Chimwaga Nzuguni
(hekta 300) na msitu wa Mbwenzelo (hekta 3,500) pamoja na vilima vya
Image na Nyankali.
“Katika
kutimiza malengo hayo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Serikali
imeendelea kutoa elimu ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu hususan
miti adimu ya asili na makao ya wanyamapori mbalimbali katika kata nane
za Ipala, Nzuguni, Kikombo, Ng’ong’ona, Chahwa, Zuzu, Hombolo na Kikuyu
Kaskazini ambapo kila kata imepewa lengo la kupanda miti isiyopungua
40,000,” amesema.
Kuhusu
zoezi la upandaji miti, Waziri Mkuu amesema miche 34,000 yenye thamani
ya sh. milioni 34 ilitolewa bure katika kata mbalimbali na kupitia mradi
wa TASAF miche mingine 138,000 inaendelea kusambazwa kwa wananchi. “Kwa
sasa, Manispaa ya Dodoma inaendelea na maandalizi ya kuotesha miche
mingine 200,000 kwa ajili ya msimu ujao,” ameongeza.
Ametumia
fursa hiyo kuwashukuru Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bonde la Wami
Ruvu, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao kwa kushirikiana na Manispaa
ya Dodoma wamefanikisha upandaji wa miche 79,000 katika maeneo ya UDOM,
Mzakwe, Iseni Park, Nala na Mahomanyika.
Katika
kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelevu, Waziri Mkuu
ameziagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe zinaandaa miche ya
kutosha na kuweka utaratibu wa kila kaya kupanda na kutunza miti
isiyopungua mitano.
“Taarifa
za utendaji na maendeleo za Halmashauri zote zioneshe mafanikio
yaliyopatikana kutokana na zoezi la upandaji miti. Utendaji wa
Wakurugenzi na Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, utapimwa kutokana na
uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao,” amesisitiza.
