Waziri Mkuu: Akiba ya Fedha za Kigeni Imeongezeka na Kufikia dola 5.91 bilioni za Marekani
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema akiba ya fedha za kigeni imeongezeka na
kufikia dola 5.91 bilioni za Marekani kiwango ambacho hakijawahi
kufikiwa kwa takriban miaka minne kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.
Ameyasema
hayo leo Februari 9, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya
kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili
3, mwaka huu.
Amesema
mbali na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, pia thamani ya mauzo
ya bidhaa na huduma nje ya nchi imekuwa takriban dola 8.695 bilioni za
Marekani ikilinganishwa na wastani wa dola 8.828 bilioni za Marekani kwa
miaka mitatu iliyopita.
Hata
hivyo, amesema utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka ni wa
kuridhisha ambapo ukusanyaji wa mapato ulifikia Sh12.95trilioni sawa na
asilimia 82.8 ya lengo lililopangwa katika kipindi hicho.
Amesema
matumizi ya fedha hizo yameelekezwa katika kugharamia shughuli
mbalimbali za Serikali za kuhudumia wananchi na miradi ya kipaumbele
ambayo ni kuanza kwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa.
Pia
kugharamia mpango wa elimumsingi bila malipo, kugharamia mpango wa
ununuzi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi na utekelezaji wa miradi ya
usambazaji maji vijijini na mijini na usambazaji wa umeme vijijini
kupitia REA.
Miradi
mingine ni ununuzi wa meli za abiria na mizigo katika maziwa, ukarabati
na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya ndege na kujenga na kuendeleza
maeneo ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini.
“Hakika
kwa mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Rais John Magufuli
kwa uongozi wake mahiri na juhudi anazofanya za kuhakikisha kuwa
wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kuwa inatekeleza
ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa kwa
mwaka 2017/2018 yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Amesema
kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara
ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuwa na mapato endelevu
kwa ajili ya kugharamia matumizi yake.
Vilevile,
kuwa na usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato ambao utasaidia
kupanua wigo na kudhibiti ukwepaji wa kodi kupitia urasimishaji wa
shughuli za uchumi kwa kuwezesha ukuaji wa biashara katika sekta ndogo
na za kati ambazo ndiyo mihimili ya kuzalisha ajira na kukuza uchumi.
Akizungumzia
kuhusu viashiria mbalimbali vya kiuchumi, Waziri Mkuu amesema
vinaonyesha kwamba hali ya uchumi ni nzuri na pato la Taifa katika
kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 lilikua kwa wastani wa asilimia
6.8.
“Hali
hii inaashiria kwamba tuna matarajio makubwa ya kufikia lengo la mwaka
la ukuaji wa asilimia 7.0. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa
katika ukuaji huo ni habari na mawasiliano, uchimbaji madini, biashara,
ujenzi na uzalishaji viwandani,” amesema.
