MWANASHERIA MKUU WA KENYA PROFESA GITHU MUIGAI AJIUZULU
Mwanasheria mkuu wa Kenya Profesa Githu Muigai amejiuzulu baada ya kuhudumu kwa miaka sita na nusu.
Rais Uhuru Kenyatta amemshukuru Profesa Githu kwa huduma zake na sasa jaji Paul Kihara Kariuki atachukua nafasi yake.

Ujumbe wa rais Uhuru Kenyatta aktika mtandao wa Twitter
''Nimepokea kwa majuto uamuzi wa
mwanasheria mkuu Githu Muigai . Namshukuru kwa huduma yake katika
kipindi cha miaka sita na nusu. Nimemteua jaji Paul Kiharara Kariuki" ,
Rais Uhuru Kenyatta alichapisha katika mtandao wake wa Twitter.
Kabla ya uteuzi wake kuwa mwanasheria
mkuu profesa Muigai alikuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya mawakili ya
Mohammed Muigai na amekuwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika
kukabiliana na ubaguzi wa rangi.
Alikuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha
sheria cha Columbia mjini New York . Kutoka 1984 alikuwa mwanafunzi
katika chuo cha kusomea uanasheria nchini Kenya .
Vilevile alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi .
Akiwa mshauri wa serikali katika maswala
ya kisheria, Githu Muiga atakumbukwa kwa kuleta sheria za mageuzi
katika timu ya uchaguzi nchini Kenya siku chache tu kabla ya uchaguzi
kufanyika.
Katika sheria hiyo kamishna yeyote yule
katika tume ya uchaguzi alipewa nguvu za kumtangaza mshindi wa uchaguzi
iwapo mwenyekiti wa tume hiyo hayupo.
Sheria hiyo ilizua pingamizi kutoka kwa
upinzani pamoja na jamii ya kitaifa waliodai kuwa serikali haiwezi
kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi wakati ambapo uchaguzi mkuu
unakaribia.
Vilevile Githu Muigai atakumbukwa na
hatua ya kuliharamisha kundi la upinzani la NRM hatua ambayo pia
ilipingwa na viongozi wa upinzani wakisema kuwa ni hatua mojawapo ya
serikali ya kutaka kukandamiza upinzani.
Siku chache kabla ya kiongozi wa
upinzani Raila Odinga kula kiapo cha kuwa 'rais wa wananchi' , Bwana
Githu alitishia kuwa mtu atakayejaribu kula kiapo cha urais atajilaumu
mwenyewe kwa kuwa mashtaka yatakayomkabili ni ya uhaini ambao hukumu
yake ni mtu kunyongwa.
Hatahivyo Raila alikula kiapo hicho
katika bustani ya Uhuru Park katika hafla iliohudhuriwa na maelfu ya
wafuasi wa upinzani. Matokeo yake yalisababisha viongozi wa karibu
walioshiriki katika kumlisha bwana Raila Kiapo hicho kukamatwa na
kushatkiwa huku wengine wakifurushwa kutoka nchini.
Hatahivyo viongozi wengine wakuu wa upinzani hawakuhudhuria hafla hiyo.
Chanzo-BBC
