Mhagama atoa ufafanuzi muungano wa mifuko ya pensheni

Waziri wa nchi Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemevu, Jenista Mhagama  jana bungeni amewasilisha muswada  wa sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Umma wa mwaka 2018 na kupendekeza kuunganishwa mifuko ya pensheni ya PSPF, LAPF, GEPF na PPF ili kuanzisha mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii.

#Muswada huu unapendekeza kuunganishwa mifuko ya Pensheni ya PSPF, LAPF, GEPF na PPF ili kuanzisha Mfuko mmoja wa Hifadhi ya Jamii.

#Hatua ya kuunganisha mifuko ya Pensheni inalenga kukidhi kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kuhusu kuunganisha mifuko hiyo ili kupunguza gharama za luendeshaji.

#Sheria inayopendekezwa itaweka mfumo madhubuti utakaomhakikishia mwanachama kulipwa mafao ya msingi kama inavyoeleza Katiba ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania ya 1977 Ibara ya 11 (1).

#Sheria inayopendekezwa inabainisha kwa uwazi Jumla ya mafao 7 yatayolipwa na mfuko huu ikiwamo *Fao la Pensheni, Fao la warithi, Fao la Ulemavu, Fao la Uzazi, Fao la Ukosefu wa Ajira, Fao la Ugonjwa na Fao la Kufiwa.*

#Sheria inaweka utaratibu bora na ulio rahisi wa wanachama wa mifuko inayounganishwa kuhamia kwenye mfuko mpya pasipo kuathiri mafao yao na uendelevu wa mfuko mpya.

#Kuweka bayana kwamba mafao na michango ya wanachama haitatozwa kodi kama ilivyokwisha bainishwa katika sheria ya kodi.

#Kiwango cha Uchangiaji kitakuwa ni asilimia 20 ambapo mwajiri atachangia asilimia 15 na mwajiriwa atachangia asilimia 5 ya mshahara wake.

#Kuweka mfumo madhubuti utakaohakikisha mwanachama anapata mafao kwa wakati ikiwamo kwa kuutaka mfuko kumlipa mwanachama aliyekidhi vigezo mafao yake hata kama mwajiri hajawasilisha na baadae mfuko utafuatilia michango ambayo haijawasilishwa kutoka kwa mwajiri.

#Kuainisha adhabu ya tozo ya Asilimia 5 kwa mfuko utakaochelewesha mafao ya wanachama.

#Kuainisha adhabu ya tozo ya Asilimia 5 kwa mfuko utakaochelewesha mafao ya wanachama.

#Sheria hii itamwezesha mwanachama kutumia mafao yake kujipatia mikopo ya nyumba na shughuli nyingine za kiuchumi kwa riba nafuu.

#Sheria hii inaainisha kwa uwazi haki na stahili za warithi pale mwanachama au mstaafu anapofariki.

#Sheria inaondoa kilio cha muda mrefu cha wastaafu katika utumishi wa umma kuhusu kukoma kwa mafao/pensheni pale mstaafu anapofariki dunia, sheria hii inaruhusu wategemezi kuendelea kupokea mafao kwa kipindi cha miezi 36.

#Sheria inapendekeza kuboresha masharti kuhusu fao la uzazi ambapo pamoja na kupata fedha taslimu baada ya kujifungua, mwanachama pia atapata huduma za matibabu kabla na baada ya kujifungua endapo huduma hizo hazilipwi na NHIF.

#Mwanachama atakuwa na fursa ya kupata fao la uzazi mara nne katika kipindi chote cha ajira.

#Sheria inapendekeza kuanzisha kwa Fao la Upotevu wa Ajira ili kuondoa changamoto ya muda mrefu ya wanachama kujitoa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

#Mwanachama atakuwa na fursa ya kupata Fao la Upotevu wa Ajira baada ya kukidhi vigezo vilivyoainishwa ndani ya sheria.

#Vigezo ni Awe amechangia kwa kipindi kisichopungua miezi 18, awe Mtanzania, awe hajaacha kazi kwa matakwa yake mwenyewe, awe hajafika umri wa kupata pensheni, uthibitisho wa Mkurugenzi Mkuu kuwa hajaweza kupata kazi nyingine, awe hajafika umri wa miaka 55.

#Sheria hii inatoa fursa kwa mwanachama anayetumikia kifungo jela kushirikishwa juu ya namna bora ya mafao yake yatakavyotumika ikiwa ni pamoja na kutunza familia yake akiwa anaendelea na kifungo.

*Imeandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO*
Powered by Blogger.