Jaji Mutungi avionya CCM, Chadema
MSAJILI
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi, amevikumbusha vyama
vinavyoshiriki uchaguzi mdogo kuhakikisha vinatii sheria zake, sheria za
gharama za uchaguzi na kanuni zake katika kipindi hiki cha uchaguzi
mdogo katika Majimbo ya Siha na Kinondoni.
Jaji
Mtungi aliyasema hayo kupitia barua aliyoiandikia vyama hivyo juzi
kuhusu wajibu wao wa kutii sheria wakati wa uchaguzi huo.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica
Laurent, alisema vyama hivyo vimetakiwa kutii sheria hasa kwa kuepuka
vitendo vya fujo, lugha za uchochezi na matusi.
“Natambua
kuwa vyama vyenu vinashiriki katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge
na udiwani zinazoendelea katika majimbo na kata, hivyo natumia fursa
hii pia kuvipongeza vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi huo
katika tukio hilo muhimu la kidemokrasia,” ulisomeka ujumbe wa barua
hiyo kwa vyama vya siasa.
“Aidha,
naviasa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo, kuheshimu na kufuata sheria
za nchi, hasa sheria ya vyama vya siasa, sheria ya gharama za uchaguzi
na kanuni zake, kwa kuepuka vitendo vya fujo na lugha za matusi na
uchochezi,” aliongeza.
Pia
Jaji Mtungi alitoa wito kwa wanachama wa vyama vya siasa kutoa taarifa
katika mamlaka husika endapo wanashuhudia viashiria vya uvunjifu wa
sheria katika kampeni na uchaguzi badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Uchaguzi
katika majimbo ya Kinondoni na Siha unafanyika baada ya wabunge
waliokuwapo kuhama wakitokea vyama vya upinzani vya CUF na Chadema na
kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika
jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia anagombea kupitia CCM baada ya
kujiengua kutoka CUF ilhali Siha, Dk. Godwin Mollel, ambaye naye alihama
Chadema na kuhamia CCM, anagombea kupitia chama hicho.