Waziri Jafo atangaza neema Siha Wakati Akimnadi Mgombea wa CCM
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Seleman Jaffo amesema Serikali kwa sasa inatafuta Sh2 bilioni kwa ajili
ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha.
Jaffo
aliyasema hayo jana katika viwanja vya Sanya Juu wakati akimnadi
mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Godwin Mollel, ambaye
hivi karibuni alijiondoa Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia
chama tawala.
Jaffo alisema chama hicho ndicho chenye Serikali na ndicho kinachoweza kutatua changamoto na shida za wananchi.
Alisema
endapo Dk Mollel atashinda, Serikali itafanya kila liwezekanalo ili
kuhakikisha Siha inasonga mbele kimaendeleo na maisha ya wananchi
yanaboreshwa.
Jaffo
aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua Dk Mollel ili kuisukuma
Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha maisha
ya wananchi.
“Mollel
ni kiongozi makini, mpeni ridhaa ili Serikali tushirikiane naye
kuwaletea maendeleo na ninawahakikishia mkimchagua, miaka miwili
iliyobaki Siha itakuwa moja ya wilaya ambazo zitapiga hatua kubwa na
kufanya vizuri katika utekelezaji wa maendeleo,” alisema.
“Naomba
msifanye makosa maana tutashughulika na shida na changamoto zote za
wananchi, tutatatuta tatizo la maji, tutaboresha huduma za afya, elimu,
barabara na kuwafanya wananchi kupata huduma zote muhimu za kijamii.”
Akimnadi
Dk Mollel, katibu wa itikati na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole mbali
na kuwaomba wananchi wa Siha kumchagua Mollel aliwataka wanasiasa kuacha
kutumia shida za wananchi kama mtaji wa kisiasa.
“Muda
wa kufanya siasa za uwongo umepitwa na wakati, sasa tufanye siasa za
kushughulika na shida za wananchi, tuboreshe maisha na kusogeza karibu
na wananchi huduma za kijamii na tusigeuze maisha ya watu kuwa mtaji wa
kisiasa,” alisema Polepole.
Alisema
maendeleo hayana vyama, hivyo kuwataka wananchi kumchagua Dk Mollel,
ambaye amehamia timu ya ushindi ambayo ina uhakika wa kuwaletea
maendeleo.
Akiomba
kura, Dk Mollel alisema alivua gwanda ili aweze kushughulika na shida
za wananchi na hivyo akawaomba wananchi kumpa kura zote za ndio.
Aliwaambia
wananchi kuwa anatambua mchango wao wa mwaka 2015, hivyo wamrudishe
ulingoni ili akatatue changamoto zinazowakabili, ambazo alishindwa
kuzitatua akiwa upinzani.
“Natambua
mchango wenu katika ubunge nilioupata 2015, lakini mlinituma kusoma
ramani ya maendeleo na niliona nilikokuwa kulinituma katika ramani ya
vijiweni na ndio maana nimeingia huku ambapo naona ramani ya maendeleo
inasomeka vyema, hivyo nipeni kura zote ili nikatekeleze,” alisema.
Alisema
akichaguliwa Februari 17,atashirikiana na Serikali kuhakikisha
wanatatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo tatizo la maji, miundombinu
ya shule, barabara na migogoro ya ardhi.