Sababu zilizopelekea serikali kusitisha utoaji wa 'passport' za makundi
Serikali
imesitisha utoaji wa pasi za kusafiria ‘passport’ za jumla za makundi
mpaka pale utakapopatikana utaratibu rasmi na mzuri kati ya serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya nchi husika.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt Mwigulu Lameck
Nchemba kufuatia kuwepo kwa mikasa ya kunyanyaswa, kutumikishwa na
kuteswa kikatili kwa baadhi ya watanzania wanaokwenda nje ya nchi kwa
jili ya kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kazi za ndani.
“Nimezipata
taarifa hizo za mateso ya watu wetu wanaokwenda nje ya nchi kwa kazi
tofauti tofauti…. Nasimamisha utoaji wa pasport za jumla za makundu ya
vijana ambao wamekuwa wakikutana na mikasa hiyo ya kunyayaswa,
kutumikishwa, kuteswa kikatili na wengine kuwekwa rehani kwa maswala ya
dawa za kulevya. tunasimamisha mpaka pale tutakapokuwa tumeweka
utaratibu ulio rasmi na utaratibu mzuri kati ya serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na serikali ya nchi husika ambako kutakuwa na
mahitaji ya namna hiyo,” amesema Waziri Dkt Nchemba.
Waziri
Dkt Nchemba ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuwanusuru vijana
wa Tanzania kutokana na mateso na ukatili ikiwamo kuwekwa rehani kwa
madawa ya kulevya pamoja na kunyang’anywa passport na kutumikishwa.
Vilevile
Waziri Nchemba ameelza kuwa, kumekuwa na tabia ya watu kuingiza raia wa
kigeni hapa nchini na wanapowaingiza wanawafanyisha shughuli nyingine
ambazo ni tofauti na zilizopo kwenye vibali vyao, huku akiwataka wote
wanaofanya hivyo kuripoti leo, na tofauti na hapo watachukuliwa hatua
kali za kisheria.
“Wako
raia wanaoingia kwa makundi nchini kwetu, na wale wanaowaleta wanatumia
sababu tofauti wanapowaleta, na wanapoingia wanawafanyisha shughuli
tofauti na walizoombea vibali. Watu wote wanaoomba vibali na baadae
wakatumia vibali hivyo tofauti ama wakafanya majukumu mengine tofauti na
waliyoombea vibali, wanavunja sheria na watafika kwenye mkono wa
sheria,” amesema Waziri Nchemba.
“Watu
hawa naelekeza leo hihi hii waripoti kwa kamishna wa mipaka na Kamishna
wa vibali… na kama mpaka jioni watakuwa hawajaripoti, wakamatwe na
wafike kwenye mkono wa sheria, ili sheria iweze kufata mkondo wake,”
ameongeza Waziri Nchemba.