Tundu Lissu Atolewa Risasi Nyingine Mwilini Mwake
Siku
35 baada ya Tundu Lissu kusema mwili wake bado una risasi moja baada ya
kutolewa nyingine 15, jana mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema)
alisema kuwa madaktari wamemtoa kipande cha risasi kilichokuwa mwilini
mwake.
Hata
hivyo, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, ambaye alishambuliwa kwa zaidi
ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini
Dodoma Septemba 7 mwaka jana, alisema chuma hicho ni tofauti na risasi
aliyonayo mwilini, ambayo alielezwa na madaktari wa Hospitali ya
Nairobi, Kenya kuwa iko sehemu mbaya, lakini isipotolewa haiwezi
kumdhuru.
“Leo
(jana) madaktari wamenitoa kipande cha chuma katika sehemu ya makalio
ambacho nilipokuwa Nairobi (Kenya) madaktari walikiona lakini kilikuwa
ndani ya nyama wakashindwa kukitoa,” alisema Lissu
“Kipande hiki kilisogea na wamekitoa. Ni tofauti na ile risasi ambayo iko mwilini mwangu.”
Akieleza kiundani kuhusu hali yake, Lissu alisema anaendelea vizuri.
“Huu
mkono wa kushoto ambao ulikuwa na tatizo, wameunyoosha na kuufanyia
mazoezi kweli kweli na huu mguu wa kulia ambao ndio wenye tatizo,
unaendelea vyema,” alisema.
“Huku
ni mazoezi tu. Kwa siku nafanya mazoezi kwa saa nne, Naingia saa 3:00
asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi, narudi tena saa 5:00 asubuhi hadi saa
6:00 mchana. Mwisho naingia mazoezini saa 8:00 mchana hadi saa 10:00
jioni. Hiyo ndiyo ratiba yangu kwa siku.”
Alisema katika mazoezi hayo anatumia magongo maalumu pamoja na kiti cha magurudumu.
“Mfano,
huu mguu wa kulia natakiwa kuukanyagia kwa kilo 20 hadi 25 katika mzani
na mimi nina kama kilo 90. Ninapoukanyagia ninaulizwa kama unauma,
ikiwa sijasikia maumivu ina maana sijafanya kitu, kwa hiyo ni kazi
kwelikweli,” alisema.
Kuhusu muda ambao anatakiwa kufanya mazoezi hayo mpaka atakaporejea katika hali yake ya kawaida, Lissu alisema bado hajajua.
“Ah
bwana we, hapa madaktari wamegoma kunieleza hilo, lakini wameangalia
katika maungio ya goti la mguu wa kulia kuna mfupa haujaunga vizuri, ni
lini utaunga hilo sijajua,” alisema.
Mara
baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa
hawajajulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa
matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya
siku hiyo usiku.
Desemba
21 mwaka jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, Lissu
alisema madaktari wa Nairobi walimueleza kuwa risasi iliyokuwa imesalia
mwili haina madhara.
Alisema
risasi saba zilitolewa na madaktari hao, jambo lililomaanisha kuwa
risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache
baada ya kushambuliwa alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.