Uhamiaji wapewa siku tatu tu kuhama mjini
IDARA
ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa siku tatu
kwa watumishi wake walioripoti Dodoma kuhamia katika nyumba zake
zilizopo eneo la Iyumbu, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, badala ya
kung’ang’ania kuishi katikati ya mji.
Nyumba hizo 63 zenye thamani ya Sh. bilioni 3.8 zimekabidhiwa jana kwa Idara hiyo na Shirika la Nyumba (NHC).
Akizungumza
katika makabidhiano hayo, Kamishna wa Fedha wa Idara hiyo, Peter
Chogero, kwa niaba ya Kamshina Mkuu alisema serikali imeshanunua nyumba
kwa ajili ya watumishi hao hivyo hakuna sababu ya wao kuendelea kuishi
katikati ya mji wa Dodoma.
“Uhamiaji
imenunua nyumba 63 eneo la Iyumbu ambazo zimejengwa na NHC, tutashangaa
kuona watumishi wengine waendelee kuishi mjini wakati nyumba zao zipo
hapa Iyumbu,” alisema.
Alitoa
siku tatu kuanzia jana kila mtumishi aliyepangwa kuhamia kwenye nyumba
hizo awe ameingia kwa kuwa hakuna sababu ya kung’ang’ania kuishi nje ya
nyumba hizo wakati zimelipiwa na serikali.
Chongero
alisema kabla ya manunuzi ya nyumba hizo, Idara hiyo ilikuwa na nyumba
10 mjini Dodoma ambazo hazikuweza kutosheleza watumishi wote, ikiwamo
waliohamia kutoka Makao Makuu Dar es Salaam.
Alibainisha
waliamua kuongeza idadi ya nyumba ili kila mtumishi wa Uhamiaji aishi
kwenye nyumba ya serikali na kwamba wanatarajia kuongeza nyingine 40.
Naye,
Meneja Masoko wa NHC, Itandula Gambalagi alisema ujenzi wa nyumba za
Uhamiaji ulianza Desemba, 2016 katika eneo lenye ukubwa wa ekari 234 na
ni moja ya sehemu ya mji uliopangiliwa kitaalamu kwa kuzingatia sheria
na kanuni za mipango miji.
Alisema
nyumba zilizokabidhiwa Uhamiaji ni sehemu ya nyumba 150 zilizojengwa
katika mradi wa Iyumbu na tayari nyumba zilizobaki zote zimepata
wanunuzi.
Gambalagi alisema nyumba hizo zina miundombinu yote inayotakiwa.
Kwa
upande wake, mthamini wa mali za serikali, Joseph Maliti aliagiza
Uhamiaji kuingiza nyumba hizo katika daftari la mali za serikali mara
moja, ikiwa ni pamoja na thamani kwa kila nyumba.