Polisi Yaendelea Kukuna Kichwa Skata la Nabii Tito
JESHI
la Polisi mkoani Dodoma limesema bado linashauriana na vyombo vingine
juu ya hatua za kumchukulia mkazi wa Mtaa wa Ng'ong'ona katika Manispaa
ya Dodoma, Onesmo Machibya anayejiita 'Nabii Tito', ambaye anatuhumiwa
kueneza chuki ya kidini dhidi ya watu wengine.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto jana alisema bado jeshi hilo
linamshikilia Machibya (44) kwa kuwa imethibitika ana ugonjwa wa akili.
Alisema polisi inashirikiana na vyombo vingine ili kujua hatua stahiki za kumchukulia.
Aidha,
Muroto alisema jeshi hilo bado linawatafuta wake zake wawili pamoja na
kijakazi wake wanaodaiwa kushirikiana naye kueneza alichosema chuki
hiyo.
Muroto,
alisema kwa kufanya hivyo, nabii huyo ametenda kosa kwa kukiuka kifungu
cha sheria namba 129 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 na marekebisho
yake ya mwaka 2002.
Alidai pia nabii huyo anaendesha shughuli zake kinyume cha Sheria ya Jumuiya, sura ya 337 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
"Mtuhumiwa
huyu amekamatwa baada ya kurekodi vipande vifupi vya matangazo ya video
na picha vyenye maudhui ya kukashifu dini nyingine na kuleta chuki
dhidi ya watu wengine na kurusha kwenye mitandao ya kijamii; na pia
kusambaza vipeperushi kwenye maeneo ya starehe," alisema Kamanda Muroto.
Pia
alidai kuwa nabii huyo anatangaza imani ya dini inayokiuka maadili ya
nchi na kufanya hadharani vitendo visivyofaa akitumia kitabu kitakatifu
cha Biblia ambacho pia hafungamani nacho.
"Pia
anatoa tafakari za Biblia zenye upotoshaji, kufanya vitendo vya
udhalilishaji hadharani na kuchochea maovu katika jamii, anashirikiana
na wanawake wawili anaodai kuwa ni wake zake, mmoja wao akiwa ni
kijakazi," alisema Muroto.
Muroto
alisema nabii huyo alikamatwa akiwa na majoho meupe yenye misalaba
miwili yenye rangi nyeusi mbele na nyuma, vipeperushi 80, Biblia moja na
msalaba pamoja na vifaa anavyotumia kutangaza imani yake.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Juni 23, 2014 alilazwa katika Hospitali ya Muhimbili na kutibiwa magonjwa ya akili.
"Aliruhusiswa
kutoka wodini na daktari wake Dk. William na kutakiwa kurejea tena kwa
uangalizi wa tiba Julai 9, 2014 lakini hakurejea na pia mtuhumiwa
alifikishwa Hospitali ya Mirembe Dodoma kwa uchunguzi uliofanywa na Dk.
Dickson Philipo na kugundulika kuwa ni mgonjwa wa akili wa muda mrefu,"
alisema Muroto.
Alifafanua
hali ya kuwa mgonjwa wa akili lakini ameendelea kuhamasisha maovu
yaliyo kinyume na maadili ya dini zote na desturi za Watanzania huku
akionekana ni mtu mwenye akili timamu na kupata watu wanaomshabikia na
kuambatana naye.
Miongoni
mwa mahubiri ya Nabii Tito ni pamoja na kudai kuwa Biblia imeruhusu
watu kunywa pombe na waume za watu kuoa wafanyakazi wao wa ndani.