Serikali yazifutia usajili kampuni tatu
Serikali
yasitisha Shughuli za Kampuni Tatu (3) za Wakala binafsi wa huduma za
ajira hapa nchini kutokana na kukiuka matakwa ya sheria ya huduma za
ajira Na.9 ya mwaka 1999 na Kanuni zake.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa
Ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi na wadau
mbalimbali kuhusu utaratibu unaotumiwa na baadhi ya wakala binafsi wa
huduma za ajira nchini.
Kampuni
zilizofutiwa usajili baada ya kukiuka sheria ni pamoja na Sasy Solution
Company Ltd, Bravo Job Centre Agency na Competitive Manpower
International Ltd ambapo Kampuni hizo haziruhusiwi kujihusisha na
shughuli za Uwakala binafsi wa ajira nchini.
Akifafanua
Mhe. Mhagama amesema kuwa uchunguzi umebaini ukiukwaji wa taratibu za
usajili ambapo baadhi ya mawakala wamekuwa wakitumia nyaraka
zilizopatikana kwa njia isivyo halali katika kujipatia leseni za uwakala
hali iliyowawezesha kukwepa kodi na kujipatia faida.
Aliongeza
kuwa ukiukwaji wa taratibu za kisheria umeleta athari mbalimbali kwa
wafanyakazi hasa kwa wale wanaoenda kufanya kazi Mataifa ya Nje ambapo
wafanyakazi hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji
katika ajira, malipo ya mishahara na stahiki mbalimbali.
Aidha,
Mhe. Mhagama amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imesitisha mara moja
shughuli za Mawakala Binafsi wa huduma za Ajira zinazohusika na
kuwatafutia kazi wafanyakazi nje ya nchi (cross border placement) hadi
hapo Serikali itakapoleta mfumo wa kusimamia jambo hili na kutoa taarifa
kwa umma.