AJIUA KWA HASIRA YA KUKIMBIWA NA MKE
Mwanaume aitwae Anord Msafiri (44) mkazi
wa kijiji cha Nkomolo kata ya Nkomolo wilayani Nkasi mkoani Rukwa
amekutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya katani kutokana na
hasira baada ya kukimbiwa na mke wake.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa
kijiji hicho Teddy Chambala alisema kuwa marehemu alijinyonga ndani ya
nyumba yake juzi Januari 23,2018 majira ya saa 9 alasiri na majirani
walibaini kifo hicho majira ya saa 12 za jioni siku hiyo.
Aliiambia Malunde1 blog kuwa licha ya
marehemu huyo kutoacha ujumbe wowote kuhusiana na kifo chake lakini siku
chache kabla ya tukio hilo mke wake alitoroka nyumbani kwa madai kuwa
amechoka kuishi na mwanaume huyo ambaye ni mlevi na alikuwa akimpiga
mara kwa mara.
Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema kuwa
mke wa marehemu huyo alitoroka nyumbani na kuwaacha watoto wawili
aliozaa na Msafiri kitendo kilichosababisha apate usumbufu wa kuwalea na
maisha kuwa magumu.
Alisema kutokana na kitendo hicho ndipo
Msafiri alipoamua kujinyonga kutokana na ugumu wa maisha, hasira pamoja
na msongo wa mawazo kwani alibaki mpweke akiwalea watoto peke yake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George
Kyando alisema hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio hilo lakini
polisi bado wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.
Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Nkasi