Hiki ndicho amekisema Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu watu ambao wanamtusi Rais Magufuli

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amefunguka na kusema kuwa wao kama viongozi wanazidi kuimarisha huduma mbalimbali za afya ili watu ambao wanamtusi Rais John Pombe Magufuli wazidi kuwa na afya nzuri.

Makonda amesema hayo leo Januari 25, 2018 akiwa katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam alipofanya ziara na kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Alli Hapi kwa kazi nzuri anayofanya kuhakikisha masuala ya maendeleo kwa wananchi yanaonekana na kufanyika.

"Wanaoatamba na kumtukana Rais Magufuli ni kwa sababu wazima lakini wakiugua watakuja Mwananyamala, Amana, wengine wataenda Temeke, Muhimbili hata Mlonganzila kuomba matibabu, ila wakiwa wazima waache waseme wanavyotaka, sasa kazi yetu sisi kuwafanya wawe wazima, wakiwa wazima wakija kushukuru sawa na wasipokuja kushukuru basi mwenyezi Mungu anajua namna ya kubariki viongozi wetu wanaofanya kazi zao, lakini mwisho wa siku kubariki Chama Cha Mapinduzi ambacho kimetupatia viongozi waadilifu na waaminifu wanoifanya hii kazi" alisema Makonda

Mbali na hilo Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaama amesema kuwa kwa sasa wanampango wa kuingia kwenye mfumo wa matibabu kwa njia ya kadi na kudai kuwa njia hiyo itapunguza kero mbalimbali na usumbufu usio na msingi kwa wagonjwa.

"Tiba kwa kadi ni muhimu sana na tutakuja kuzindua kampeni kubwa sana hapa na tutatoa muda fulani kwamba kila mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaama lazima awe na kadi yake na kama huna kadi huwezi kupata matibabu, sasa isije kufika hiyo hatua ya kukulazimisha wakati jambo la afya ni muhimu sana" alisisitiza
Powered by Blogger.