Rais Magufuli Kuzindua Pasipoti ya Kielektroniki
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli leo
atazindua Pasipoti Mpya ya Tanzania ya kielektroniki jijini Dar es
Salaam.
Uzinduzi
huo utafanyika Jumatano, Januari 31, 2018 kuanzia saa moja na nusu
asubuhi, Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Kurasini Dar es salaam.
Hayo
yalisemwa na Mrakibu wa Uhamiaji ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Idara ya
Uhamiaji, Ali Mtanda katika mahojiano maalum na Idara ya Habari
(MAELEZO).
Mtanda
alisema kuwa Pasipoti Mpya ya Tanzania ya kielektroniki ni sehemu ya
Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao utakuwa na visa, vibali mbali mbali na
manejimenti mipakani.
Kwa kuwa teknolojia inazidi kukua, Tanzania haiwezi kubaki nyuma ndiyo maana imeamua kuingia katika masuala ya digiti.
Uzinduzi huu utahudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Marais
wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waheshimiwa, Ali Hassan
Mwinyi, Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi
wengine wa Serikali wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo kwa mujibu wa
Mtanda.
Tanzania
imekuwa mstari wa mbele katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
katika kutoa huduma zake kwa wananchi kwa njia ya mtandao. Ikumbukwe
kuwa usajili wa makampuni chini ya Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA) wamezindua usajili wa makampuni kwa njia ya mtandao,
miamala ya pesa inafanyika kwa kiwango kikubwa kwa njia ya mtandao na
kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi ikiwepo kulipa kodi mbali
mbali.