Raila Odinga hatarini kushtakiwa kwa uhaini
MAMLAKA za Kenya, jana zilizima vituo
vya televisheni kuzuia matangazo 'live' ya sherehe za kuapishwa kwa
kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, ambaye alisusia uchaguzi wa marudio
wa mwaka jana uliobishaniwa.
Alijitangaza kuwa "rais wa watu" mbele ya maelfu ya wafuasi wake katika mji mkuu wa Nairobi.
Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti, mwaka jana, yalibatilishwa kutokana na madai ya ukiukwaji wa kanuni.
Uhuru
Kenyatta alishinda uchaguzi wa marudio Oktoba, lakini Odinga
hakushiriki, hivyo Kenyatta aliapishwa kuongoza muhula wa pili Novemba,
mwaka jana.
Alivionya
vyombo vya habari kutotangaza shughuli ya jana na mwanasheria wa
serikali alisema kufanya hafla hiyo ni kosa la uhaini.
Hata hivyo, vituo vikuu vya TV vilionyesha tukio hilo kupitia mitandao yake ya kompyuta, kwenye YouTube na Facebook.
Akiwa
ameshika Biblia mkono wake wa kulia katika bustani ya jijini Nairobi,
Odinga alitangaza kuwa anajibu "wito wa ngazi ya juu kuchukua ofisi ya
rais wa watu wa Jamhuri ya Kenya."
Watu
wamechoshwa na wizi wa kura katika uchaguzi na tukio hilo lilikuwa
hatua kuelekea ujenzi wa demokrasia sahihi katika nchi hiyo ya Afrika
Mashariki, Odinga aliuambia umati uliokuwa ukishangilia.
Aliyekuwa mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, hakuwapo kwenye hafla hiyo. Odinga alisema ataapishwa siku nyingine.
Akizungumza
awali na televisheni ya Kenya ya KTN, Odinga alisema kufungwa kwa
vyombo vya habari "kumethibitisha kuwa tumeporomoka kufikia kiwango cha
Uganda", ambayo ilisimamisha matangazo ya vyombo vya habari wakati wa
uchaguzi mwaka 2016.
"Kuapishwa
kwake" kulikuwa na lengo la "kuonyesha dunia kuwa tunachofanya ni
halali kisheria, kikatiba na kitu ambacho huwezi kukielezea hata kidogo
kuwa mapinduzi", alisema zaidi.
Vituo vitatu binafsi vya televisheni - NTV, KTN na Citizen TV - vilizima matangazo kuanzia saa 3:10 asubuhi.
Citizen
TV iliiambia BBC kuwa mamlaka za serikali ziliwalazimisha kuzima
matangazo kutokana na mipango ya kuonyesha mkusanyiko huo.
Watazamaji
wa KTN walishuhudia vioo vya luninga zao vikishika rangi nyeusi wakati
mtangazaji akisoma taarifa kutihibitisha kuwa mamlaka ya mawasiliano
ilikuwa ikizima matangazo.
Kuzimwa kwa 'signo' ya matangazo ya vyombo vya habari si jambo la kawaida hapa Kenya.
Palikuwa
na wasiwasi jana huku baadhi ya shule katika mji mkuu wa Kenya
zikifungwa kwa sababu ya tukio hilo, na watu kutojua nini kingetokea.
Polisi awali walizingira viwanja hivyo, lakini baadaye wakaondoka.
Chanzo: BBC