Wanne wafariki kwa kufukiwa na kifusi Arusha
Wachimbaji
wanne wamefariki na mmoja yupo mahututi baada ya kuangukiwa na Ngema
walipokuwa wakipakiza changarawe kwenye gari katika machimbo ya
changarawe yaliyopo katika mlima Murieti katika jiji la Arusha.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha jana Januari 30
kuhusu kutokea tukio hilo mchana, katika eneo ambalo ni machimbo ya
muda mrefu ya changarawe.
Miili
ya watu watatu tayari imetambulika ambao ni Yusuph Mohamed Kamwende(35)
Athuman Hussein umri wake haujatambulika na Richard Kishimbo(57).
"Bado
mwili wa marehemu mmoja haijafahamika na tunaomba watu kufika chumba
cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya mkoa Mount Meru kutambua ndugu
zao" alisema Kamanda.
Hata
hivyo, alitoa wito kwa maafisa madini kwenda mara kwa mara kwenye
maeneo ya machimbo ili kutazama usalama wa maeneo hayo ili kuondoa
majanga.
"Pale inaonekana ngema moja ilikuwa imelegea sasa wao wakiwa wanachimba changarawe ndipo iliwadondokea na kuwafukia" alisema
Mmoja
wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lemanya amesema wakati watu hao
wakichimba, ilisikika mlio wa kuanguka ngema na waliona wakiangukiwa.
"Wao
walikuwa wameingia chini ya ngema na kuanza kukata miamba na ndipo
mtikisiko ulitokea na kufanya kumeguka kwa ngema na kuwaangukia"Amesema
Hata
hivyo hili ni tukio la pili ndani ya miaka mitatu kutokea ambapo mwaka
juzi pia machimbo hayo yalifungwa baada ya kusababisha vifo kutokana na
wachimbaji kuangukiwa na ngema.