Rais Magufuli akutana na Mjumbe Maalum wa Rais Kagame
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 25 Januari, 2018 amekutana na Mjumbe Maalum wa Rais wa Rwanda na
aliyewahi kuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Donald
Kaberuka na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya
Tanzania na umoja wa Afrika (AU).
Baada
ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Dkt. Kaberuka
amesema uchumi wa Tanzania unakua vizuri na amempongeza Mhe. Rais
Magufuli kwa jinsi anavyosimamia ukuaji wa uchumi huo.
“Nimefurahi
sana jinsi Tanzania inavyokwenda mbele, maendeleo yanakwenda kwa kasi
na Mhe. Rais anafahamu kabisa kwamba katika Afrika nchi zetu zinahitaji
kuwa na uchumi bora, ningependa kumpongeza Mhe. Rais na Watanzania wote
kwa kazi nzuri wanayofanya” amesema Dkt. Kaberuka.
Dkt.
Kaberuka amesema katika mazungumzo hayo pia amewasilisha ujumbe wa Rais
wa Rwanda Mhe. Paul Kagame ambaye kuanzia mwezi huu atakua Mwenyekiti
wa Umoja wa Afrika (AU), na ndiye aliyekabidhiwa majukumu ya kufanya
mabadiliko ndani ya umoja huo.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Zimbabwe hapa nchini
anayemaliza muda wake Mhe. Edzai Chimonyo na kumpongeza kwa uwakilishi
mzuri alioufanya kwa miaka 10 aliyoiwakilisha Zimbabwe hapa nchini.
Mhe.
Rais Magufuli amemuomba Mhe. Chimonyo kumfikishia salamu za pongezi
Mhe. Emmerson Mnangagwa kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zimbabwe na
amemuhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri
wa kihistoria na kidugu uliopo kati yake na Zimbabwe.
“Naomba
umwambie Mhe. Rais Mnangagwa kuwa namkaribisha atembelee Tanzania na
namtakia heri katika majukumu yake, natarajia ataendeleza uhusiano na
ushirikiano wetu ili tuweze kujiimarisha zaidi kiuchumi kwa manufaa ya
nchi hizi mbili” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Chimonyo ameshukuru kwa ushirikiano mkubwa alioupata katika kipindi
chake cha Ubalozi hapa nchini na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
namna anavyoiongoza nchi, huku akitaja baadhi ya mambo yanayofanywa kwa
mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa, ujenzi wa
miundombinu hususani barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
Mhe.
Chimonyo ambaye alikuwa kiongozi wa Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha
nchi zao hapa nchini na Kaimu Kiongozi wa Mabalozi wote wanaowakilisha
nchi zao hapa Tanzania amesema Mabalozi hao wanafurahishwa na wanaunga
mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli ikiwemo
kuhamia makao makuu Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Januari, 2018