Mwalimu Atiwa Mbaroni Kwa Lugha Ya Matusi Mtandaoni
JESHI
la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari
Mkolani, Deogratius Kisandu, akidaiwa kutumia lugha ya matusi, kejeli na
kudhalilisha katika ukurasa wake wa Facebook.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed
Msangi, alisema Kisandu alikamatwa jana baada ya kuwapo taarifa kuhusu
kuonekana ujumbe wa matusi na lugha zisizofaa katika ukurasa wake ya
Facebook.
Alisema
walimfuatilia mtuhumiwa na kumkamata akiwa na simu yake ambayo huitumia
kupeleka na kuandika matusi hayo kinyume na Sheria Namba 4 ya Makosa ya
Mtandao ya Mwaka 2015.
“Polisi
bado wanaendelea na na mahojiano na upelelezi dhidi ya mtuhumiwa.
Utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
“Taarifa zinaonyesha kuwa mtuhumiwa amewahi kushtakiwa kwa makosa kama hayo kipindi cha nyuma,” alisema Kamanda Msangi.
Kamanda
amewataka vijana wanaotumia mitandao ya jamii kuacha kwa sababu ni
kosa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.
Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema alipokea malalamiko kutoka
kwa wananchi siku mbili zilizopita kuhusu lugha ya kudhalilisha, matusi
na kejeli inayotumiwa na Kisandu ambaye pia ni mtumishi wa umma,
katika ukurasa wake wa Facebook.
“Tumetumia
siku mbili mpaka kumpata Kisandu. Mwanzoni nilifikiri labda haya mambo
yanafanywa na mtu ambaye si raia wa Tanzania lakini katika mahojiano
amekiri yeye ni Mtanzania.
“Kwa kweli lugha anayoitumia ni ya kudhalilisha, matusi na kejeli na haifai kutumiwa kutokana na utamaduni wetu,” alisema.
Meneja
wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Lawi Odiero,
alisema sheria ipo na inakataza matumizi mabaya ya mitandao na kwa
kuwa kesi hiyo ipo polisi atatoa ushirikiano unaohitajika kusaidia
uchunguzi.