Mawaziri Wa Fedha Na Mipango Wa Tanzania Na Rwanda Wakutana Kujadili Mradi Wa Ujenzi Wa Reli Ya Isaka- Kigali
Benny Mwaipaja, WFM
Mawaziri
wa Fedha na Mipango wa Tanzania na Rwanda wamekutana Jijini Dar es
Salaam kujadili namna ya kupata fedha za Ujenzi wa Reli yenye Kiwango
cha Kimataifa (SGR) kutoka Isaka Shinyanga hadi Kigali Rwanda ikiwa ni
mwendelezo wa mikutano kuhusu suala hilo iliyoanza kuanzia Januari 20,
2018.
Katika
Mkutano huo wamejadili kuhusu njia ambayo inaweza kuwa rahisi kupata
fedha ikiwemo ya kutumia Sekta binafsi, Serikali kukopa au kumweka
mwekezaji ambapo wamekubaliana kupitia upya taarifa zilizo wasilishwa
mezani za pande hizo mbili na kufanya maboresho na pia kuzungumza na
Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya
Maendeleo ya Afrika kwa pamoja ili wakati wa kikao kijacho waweze
kujadili suala hilo kwa kuangalia vigezo na masharti ya kupata fedha.
Kikao
hicho ambacho ni cha watalamu kimewakutanisha Waziri wa Fedha na
Mipango wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri kutoka
Rwanda Mhe. Gatete Claver pamoja na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania,
Eugene Kayihura na Makatibu wakuu wa wizara hizo na wajumbe wengine.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania Bw. Doto James na
mwenzake wa Rwanda Bw. Caleb Rwaungaza, wamesaini maagizo hayo ya
Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji.
Ikumbukwe
kuwa mapema mwezi huu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais
wa Rwanda Paul Kagame walikubaliana kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa
Reli kutoka Isaka Shinyanga hadi Kigali Rwanda na wakatoa maagizo ya
kuanza utekelezaji kwa kuangalia namna ya kupata fedha za mradi huo.