Serikali Yauza Meno Ya Viboko Kwa Sh.30,900,000/= Katika Mnada Wa Hadhara Jijini Dar Es Salaam
Serikali
kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanya
mnada wa hadhara wa kuuza meno ya viboko vipande 12,467 yenye uzito wa
kilo 3,580.29 katika ofisi zake ndogo katika Jengo la Mpingo,
jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya makampuni 19 yenye leseni daraja
la kwanza yameshiriki katika mnada huo.
Mnada
huo umefanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango
ambapo kampuni ya On Tours Tanzania Limited imeibuka mshindi kwa kwa
kununua meno hayo kwa jumla ya shilingi 30,900,000/=
Awali
akizungumza katika mnada huo, Mwenyekiti kutoka Wizara ya Fedha na
Mipango, Karerema Kwaleh aliwataka wafanyabiashara kuzingatia masharti
mnada huo.
Ambapo
Karerema alimtaka mfanyabiashara yeyote atakeibuka mshindi kulipia
asilimia ishirini na tano (25%) ya bei papo hapo na asilimia sabini na
tano (75%) italipwa yote katika muda wa siku kumi na nne (14) baada ya
mnada.
Kufuatia
sharti hilo baada ya kutangazwa kwa mshindi, Mwakilishi kutoka
Kampuni hiyo, Grey Kilas aliweza kulipia asilimia kiasi hicho cha
asilimia ishirini na tano (25%) papo hapo na asilimia sabini na tano
(75%) atailipia ifikapo Februari 11, 2018.
Wakati
huohuo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TAWA, Mabula Misungwi amewatoa
wasiwasi wananchi kuwa biashara hiyo haiwezi kuchochea ujangili kwa
vile meno hayo yanauzwa kwa wafanyabiashara wale tu wenye leseni za
nyara daraja la kwanza
Mabula
amesema meno hayo yalianza kukusanywa tangu mwaka 2004 na huko nyuma
serikali ilikuwa ikiyauzia makampuni yenye leseni lakini kwa mwaka huo
wameanza utaratibu mpya wa kuuza meno hayo kwa njia ya mnada.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Grey Kilas ameishukuru
wasimamizi wa mnada huo kuwa umeendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu na
umetoa fursa kwa kila mmoja wao
Akizungumzia
kuhusu soko, Kilasi amesema meno hayo huuzwa nchini Japan, Marekani
na Hongkong ambapo hutumika katika kutengenezea mapambo kama vile stempu
pamoja na vishikizo vya nguo.
Itakumbukwa kuwa kwa mara mwisho biashara hiyo ya kuuza meno ya viboko ilifanyika mwaka 2004.