CCM YAPIGA MARUFUKU WANAFUNZI KUVAA VIMINI, MITEPESHO NA KUNYOA VIDUKU ARUSHA
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Meru mkoani
Arusha, imesema ni marufuku wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari
kwa wasichana kuvaa sketi fupi na wavulana kunyoa viduku, kuvaa suruali
chini ya makalio ili kulinda na kutunza maadili ya Kitanzania.
Pia jumuiya hiyo imempongeza Rais John Magufuli kwa kupiga marufuku
wazazi kuchangishwa michango mbalimbali kwa shule za serikali za msingi
na sekondari nchini. Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa
jumuiya hiyo wilayani Meru, Simon Kaaya jana wakati wa ziara yake ya
kikazi alipotembelea shule za msingi na sekondari, kwenye Kata ya
Ambureni.
Alisema baadhi ya shule walimu walikuwa siyo waadilifu ambapo walikuwa
wanachangisha michango hiyo wakati mwingine hata kwa ajili ya chai za
walimu. Kwa mujibu wa Kaaya, kuondolewa kwa michango hiyo kumesaidia
wazazi kupata faraja kubwa na kuishukuru serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Dk Magufuli anayehangaika na shida za wananchi wanyonge.
Kuhusu sare za shule za wanafunzi wilayani humo kutokidhi maadili ya
kitanzania, Mwenyekiti huyo aliwataka wasimamie kikamilifu kuhakikisha
hakuna wanafunzi wa kike wanaovaa sketi fupi za mlegezo au wavulana
wanaovaa suruali mlegezo zilizobana miguuni pamoja na kunyoa kiduku.
“Sisi kama wazazi jukumu letu kubwa ni kuhakikisha maadili mema
yanazingatiwa haswa na watoto wetu kwa ajili ya kutunza heshima ya nchi
yetu.
Tutaisimamia serikali wilayani hapa kuhakikisha inachukua hatua kali za
kisheria dhidi ya wanafunzi wote wanaovaa nguo ambazo hazina heshima.”
Alisema jumuiya ya wazazi moja ya jukumu lake kubwa ni kutoa malezi bora
kwa jamii nzima ikiwemo watoto na vijana na kwamba ni jukumu lao
kuhakikisha watoto na viajana wanakuwa na maadili mema katika jamii
inayowazunguka.
Chanzo- Habarileo