ATUPWA JELA KWA KUJIFANYA MWANDISHI WA HABARI WA TBC
Mahakama ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa
imemhukumu Michael Paul(32) mkazi wa Mazwi mjini Sumbawanga kutumikia
kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kujifanya ni mwandishi wa habari
ambaye anafanya kazi katika shirika la utangazaji la taifa(TBC) mkoani
humo.
Akisoma hukumu hiyo leo hakimu wa
mahakama hiyo Ramadhani Rugemalila alisema kuwa kutokana na mtuhumiwa
kukiri kosa anahukumiwa kwenda jela ili iwefundisho kwa watu wengine
wenye tabia kama hiyo.
Awali mahakamani hapo mwendesha mashtaka
wa polisi Hamimu Gwelo aliiambia mahakama kuwa mnamo siku ya Januari 22
mtuhumiwa alifika katika kikao kilichokuwa kikiendelea katika wilaya ya
Nkasi na kujitambulisha kuwa yeye ni mfanyakazi wa TBC wakati akijua
wazi kuwa anadanganya.
Baada ya utambulisho huo wajumbe wa
kikao hicho walimtilia shaka na kisha kumuomba mkuu wa polisi wa wilaya
hiyo amuhoji kwa kuwa wanamfahamu mwakilishi wa TBC mkoani humo.
Mkuu wa polisi huyo alifika na kumkamata
mtuhumiwa na kumfikisha kituo cha polisi na kisha kuwasiliana na
mwakilishi wa TBC mkoani Rukwa Nswima Ernest ambapo alikana kumfahamu
wala kufahamu taarifa zake.
Aliendelea kuiambia mahakama kuwa baada
ya mtuhumiwa kubanwa na jeshi la polisi alikiri kuwa alifanya hivyo ili
ajipatie kipato kutokana na ugumu wa maisha unaomkabili.
Baada ya Paul kufikishwa mahakamani
alikiri kutenda kosa hilo na kumuomba mahakama imsamehe kwani hatarudia
tena kutenda kosa hilo, utetezi uliopingwa na mwendesha mashtaka wa
polisi.
Ndipo mahakama hiyo ilimuhukumu kwenda jela miezi sita ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama yake.
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Nkasi