Wanachama 113 Wajitokeza Kuwania Uenyekiti UVCCM
Wanachama
wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) 113 kutoka bara na visiwani
wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti Taifa katika uchaguzi
utakaofanyika mwaka huu, idadi ambayo haijawahi kutokea tangu kuanzishwa
kwa umoja huo.
Kwa
sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Mbunge wa Donge Visiwani Zanzibar,
Sadifa Juma Khamis ambaye alichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka
2012.
Akizungumza
jana Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamidu alisemma wajumbe wa
Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM linafanya usahili wagombea
waliomba nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema
usahili huo unafanyika kwa waliomba kugombea wa nafasi za mwenyekiti,
makamu, wajumbe watano wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC), wajumbe watano
wa baraza kuu la umoja huo Taifa na wajumbe wa kuwakilisha jumuiya hiyo
katika jumuiya nyingine za chama.
Alisema
zoezi hilo ambalo limeanza tangu Aprili limefanikisha kupatikana kwa
viongozi mbalimbali wa ngazi za shina hadi wilaya na kwamba
kinachofanyika hivi sasa ni mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi za
kitaifa.
“Vijana
113 wamejitokeza kuomba nafasi ya uenyekiti. Huu utakuwa ni uchaguzi wa
kihistoria kati ya chaguzi zote zilizowahi kufanyika tangu mwaka 1978
ilipoanzishwa jumuiya hii mwaka huu. Kwa maneno mengine tumevunja
rikodi,”alisema.
Alisema
kwa upande wa nafasi ya umakamu mwenyekiti waliomba kugombea ni 23
wakati ujumbe wa Nec 118 wanachuana kugombea nafasi tano zilizopo
kikatiba.
Shaka
alisema jumla ya wagombea ambao wanawafanyiwa usahili katika kikao cha
Kamati ya Utekelezaji wa baraza la Kuu la UVCCM ni 375 huku nafasi ya
uenyekiti Taifa ikiongoza kwa waombaji wengi katika zoezi hilo.
Kwa
mujibu wa Shaka, Kamati ya utekelezaji ni kikao cha awali ambacho
kitatoa mapendekezo kwa Baraza Kuu la Taifa la umoja huu ambalo
litakutana Oktoba 17 kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya kamati hiyo.
“Baraza
Kuu litakutana hapa hapa Dodoma kwa ajili ya kupokea na kupendekeza
nafasi zilizoombwa katika mikoa na Taifa. Sisi (Baraza Kuu la umoja huo)
tunapendekeza kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa,”alisema .
Kwa
mujibu wa utaratibu CCM kikao kitakachowachuja wagombea wa nafasi zote
ambazo zinauwakilishi wa chama taifa ni Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
inayoongozwa na Mwenyekiti wake wa Taifa Dk John Magufuli.
Akizungumzia kuhusu chaguzi zilizopita za mashina hadi wilaya, Shaka alisema kuwa mambo yamekwenda vizuri katika chaguzi zote.
Alijitapa
kuwa chama chao siku zote kimekuwa kikisimamia haki na usawa ili vijana
waweze kupata fursa kwa nafasi wanazoziomba katika chaguzi mbalimbali
nchini.
“Katika
ngazi wilaya kuna changamoto mbalimbali kwenye uchaguzi ambazo
zimejitokeza lakini jumuiya hii inaongozwa na kanuni na katiba ya chama
chetu kwa hiyo tumeagiza viongozi wetu kuhakikisha kuwa wanashughulikia
malalamiko yaliyojitokeza,”alisema
Alisema
malalamiko yaliyojitokeza katika chaguzi hizo ni pamoja na hofu kuwa
kuna wagombea wamezidisha umri na dhana ya kutumia rushwa.
Hata
hivyo, alisema chama hicho kimekuwa kikikemea vitendo vya rushwa na
hivyo itakapodhibitiki uvunjaji wa kanuni watachukua hatua zinazopaswa
kuchukuliwa.
“Hatutadharau malalamiko yoyote yake, yote yatashughulikiwa na atakeyabainika kuvunja kanuni hatua zitachukuliwa,”alisema