Watu 7 wa familia moja wafariki kwa ajali
Watu
7 wamefariki papo hapo na wengine 14 kujeruhiwa, baada ya gari
walilokuwa wakisafiria aina ya Noah kugongwa na lori la mizigo wakitoka
kwenye sherehe ya harusi wilayani Hanang mkoani Manyara.
Ajali
hiyo ambayo imetokea usiku wa Oktoba 14, 2017 imehusisha Noah yenye
namba za usajili T 744 DJQ, likiwa limebeba watu wa familia moja,
kugongwa na lori aina ya semi trailer lenye namba za usajili T449 CDR
mali ya kampuni ya Lake Hill Paradise ya Singida, na kuleta majonzi na
simanzi kwa ndugu wa marehemu.
Licha
ya watu walioshuhudia, manusura wa ajali hiyo ambaye ndiye bwana harusi
aliyetoka kufunga ndoa, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari
hilo Bwana Wilson Simba ambaye pia amefariki, kutokuwa makini
barabarani kabla ya kuchepuka upande mwengine.
Kamanda
wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Manyara, Bi. Mary Kipesha,
amekiri kuwa uzembe uliosababishwa na dereva ndio uliosababisha ajali
hiyo na kupoteza watu wakiwemo yeye mwenyewe, na dereva wa lori ambaye
amekimbia kushindwa kuchukua hatua za haraka kuidhibiti.
Mganga
wa zamu wa hospitali ya Tumaini Hanang, Bwana Chaokiwa Msangi, amesema
wamepokea miili hiyo 7 na kuihifadhi chumba cha maiti, huku mmoja wa
majeruhi ambaye ndiye bibi harusi akipewa rufaa ya kwenda hospitali ya
Haydom, kwa matibabu zaidi.