Waziri awafukuza kazi maafisa wa serikali idara ya Maendeleo ya Mazao
Waziri
wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara ya
Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kuwafukuza kazi maafisa watatu wa idara
ya Maendeleo ya Mazao katika sehemu ya pembejeo ambao wamebainika
kuhusika moja kwa moja na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa sheria,
Kanuni na taratibu zilizowekwa.
Akizungumza
na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita Mhe Tizeba
alisema kuwa kufukuzwa kazi kunajiri kutokana na ukosefu wa umakini na
usimamizi mzuri wa sheria ya ununuzi wa Umma ikiwemo kusababisha
kuchapishwa kwa vocha za pembejeo zenye thamani ya Tshs 78,054,970,000
ambazo ni zaidi ya bajeti halisi iliyotengwa kwa ajili ya ruzuku ya
pembejeo kwa kiasi cha Tshs 42,587,419,200.
Watumishi
waliofukuzwa kazi ni Bw Shenal S. Nyoni aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi
wa kitengo cha pembejeo, Aliyekuwa Afisa kilimo Daraja la I Bw Michael
G. Mayabu na Bw Franks F. Kamhabwa.
Waziri
Tizeba ametumia mamlaka hayo mara baada ya kupitia taarifa ya waraka wa
mkakati wa utekelezaji na Usimamizi wa utoaji wa Ruzuku za pembejeo za
kilimo kwa wakulima kwa kutumia vocha wa mwaka 2015/2016 ambapo pamoja
na mambo mengine uliainisha utaratibu wa usimamizi wa zoezi la utopaji
wa ruzuku ambao ulilenga kuleta ufanisi katika utekelezaji wake.
Wakati
wa utekelezaji wa zoezi la usimamizi wa mpango wa Ruzuku za Pembejeo
katika Msimu wa mwaka 2014/2015-2015/2016 kulijitokeza tuhuma mbalimbali
zilizohusu ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na watumishi wa serikali Za
Mitaa zilizohusika kwenye Mpango wa Ruzuku, watumishi hao walituhumiwa
kushirikiana na Mawakala waliokuwa wamepewa dhamana ya kusambaza
pembejeo katika kuhujumu mpango huo serikalini.
Ili
kubaini ukweli wa tuhuma hizo pamoja na uhakiki uliofanywa na wizara ya
fedha na Mipango kuthibitisha uhalali wa madeni ya mawakala, Mwezi
Aprili, 2017 Wizara ya Kilimo ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo
kuwasimamisha kazi watumishi watano wa idara ya maendeleo ya mazao,
Sehemu ya pembejeo waliohusika kusimamia mpango wa Ruzuku za pembejeo za
kilimo.
Aidha,
Mwezi Mei, 2017 wizara ya kilimo iliunda kamati ya uchunguzi ili
kuchunguza tuhuma zilizowahusu watumishi hao waliosimamishwa kazi.
Katika
hatua nyingine Mhe Dkt Tizeba amemuagiza katibu mkuu wa Wizara ya
kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kuwasimamisha kazi watumishi wengine
watatu ambao ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao Bw Twahir S.
Nzallawahe, Mkurugenzi wa Kitengo cha ununuzi na Ugavi Bw Burhan A.
Shaban, na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa kitengo cha pembejeo Bw Canuth
Komba.
Zaidi
ya shilingi 29,977,114,700 zingepotea kama umakini usingekuwa mkubwa
katika uhakiki kwani katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 serikali
ilitenga kiasi cha shilingi 35,467,550,800 kwa ajili ya pembejeo za
kilimo na mara baada ya zoezi la utoaji ruzuku ilibainika kuwa deni
lililowasilishwa serikalini na mawakala ilikuwa ni kiasi cha shilingi
65,444,665,500.
Sambamba
na hayo Mhe Waziri Tizeba aliviomba vyombo vya dola kuchunguza zaidi na
kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya watumishi na watu wote
waliohusika katika ngazi za halmashauri na mawakala wote waliofanya
udanganyifu kwa lengo la kuisababishia serikali hasara.