Serikali kununua vichwa vya treni vilivyotelekezwa bandarini
Serikali imesema ipo katika mchakato wa kuvinunua vichwa 13 vya treni ambavyo vilitelekezwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo
jana Ijumaa wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa mashine za ukaguzi
wa mizigo(Scanners) zenye thamani ya Sh27 bilioni kwa ajili ya kuongeza
ulinzi na udhibiti wa mapato kwenye bandari hiyo.
Profesa
Mbarawa alisema Serikali imeunda timu ya wataalamu 11 kwa ajili ya
kufanya tathmini ya ubora pamoja na thamani ya fedha ya vichwa hivyo na
baada ya kukamilika watafanya makubaliano na mmiliki wa vichwa hivyo
ili kuvinunua.
Julai
mwaka huu katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwaajili ya upanuzi
wa bandari hiyo Rais John Magufuli alisema ana taarifa ya vichwa vya
treni vilivyoshushwa bandarini hapo lakini mmiliki wake hajulikani huku
akisisitiza kuwapo kwa mchezo mchafu.
Utata
huo uliibuka kufuatia Shirika la Reli Tanzania(TRL) kununua vichwa
hivyo kupitia mkataba wake na kampuni ya EMD ya Marekani na utengenezaji
ukafanywa na kampuni ya DCD ya Afrika Kusini huku taratibu za ununuzi
zikidaiwa kukiukwa.
Hata
hivyo tayari Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko
alishaeleza kuwa vichwa hivyo vina nembo ya TRL lakini vilizua mgogoro
baada ya kubainika kuwa mchakato wa ununuzi haukuwa sahihi.
Lakini
kwa mujibu wa taarifa iliyowahi kutolewa kwa vyombo vya habari na TRL
Machi 23, 2015 ilibainisha kuwa vichwa viwili kati ya 15 vya treni
vilivyonunuliwa na shirika hilo vilipokelewa katika Bandari ya Dar es
Salaam Machi 21, 2015.
Taarifa
hiyo ilisema vichwa hivyo vimetengenezwa nchini Afrika Kusini na kwamba
ununuzi huo umegharimu kiasi cha Sh70.9 bilioni ambazo zote
zilishalipwa.