MAHAKAMA YAAMUA ALIYEKAMATWA KWA KUDAI MUGABE NI ‘MZEE' APEWE DHAMANA
Mahakama
ya Zimbabwe imeamua kumpa dhamana mfanyabiashara mdogo (machinga)
aliyekamatwa kwa tuhuma za kumtukana Rais Robert Mugabe kuwa ‘ni mzee
asiye hai na anayeota ndoto za mchana’.
Mahakama
hiyo imemuachia mfanyabiashara huyo ambaye ni mwenyekiti wa umoja wa
wafanyabiashara wadogo (wamachinga) nchini humo, Sten Zvorwadza kwa
dhamana ya $200.
Zvorwadza, alishtakiwa kwa kosa la kumtukana Rais na kudharau Mamlaka halali ya Rais.
Mwenyekiti
huyo wa wamachinga alikamatwa baada ya kukaririwa na vyombo vya habari
akilaani amri ya Rais Mugabe ya kuwaondoa wamachinga wote kwenye mitaa
ya jiji la Harare na kuwahamishia katika maeneo waliyotengewa kwa lengo
la kulifanya jiji hilo kuwa safi kuliko majiji yote.
Gazeti
la Daily News la Zimbabwe limemkariri Zvorwadza akieleza kuwa, “kama
sekta isiyo rasmi hatutasikiliza upuuzi. Mugabe ni mzee na anaota ndoto
za mchana.”
“Mugabe
anapaswa kuheshimu kazi ya sekta zisizo rasmi. Wazimbabwe wanapaswa
kuelewa kuwa Mugabe ni mzee na ni mtu anayetembea lakini ameshakufa,”
aliongeza.
Gazeti la Harald la nchi hiyo limeripoti kuwa wamachinga wote wameondolewa mitaani na jeshi la polisi kutekeleza amri ya Rais.