Rais Magufuli Arejea Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe
15 Oktoba, 2017 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar ambako
jana alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa
Uhuru, kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere
na wiki ya vijana zilizofanyika katika uwanja wa Amaan Mjini Magharibi.
Katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mhe. Rais Magufuli
ameagwa na viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wakiongozwa na Mkuu wa
Mkoa huo Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud.
Kabla
ya kuondoka Ikulu Zanzibar Mhe. Rais Magufuli amekula chakula cha
mchana na wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka huu walioongozwa na Amour
Hamad Amour na kuwahakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi taarifa ya
Mwenge waliyoiwasilisha kwake katika sherehe za jana.
“Mlipokuwa
mkikimbiza Mwenge wa Uhuru nilikuwa nafuatilia miradi mliyokuwa
mnatembeleana maelekezo mliyokuwa mkitoa, sehemu zote mlizobaini kuwepo
kwa dosari ninawahakikishia kuwa tutazifuatilia na kuchukua hatua”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli amesema anatambua uzalendo waliouonesha wakati wote wa
kukimbiza Mwenge wa Uhuru na amewasihi kuendeleza maadili na uzalendo
huo kwa manufaa ya taifa.
Kwa
upande wao wakimbiza Mwenge hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
heshima kubwa na upendo aliyowaonesha, kwa kupokea taarifa yao na
kuahidi kuifanyia kazi na pia kuwaalika kula nao chakula cha mchana kwa
kuwa hii imekuwa ni historia ya kipekee kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru
hapa nchini.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
15 Oktoba, 2017