Askofu ataka Rais Magufuli kuungwa mkono
Askofu
wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Agustino Shao amewataka
Watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua anazochukua kurekebisha mambo muhimu
kwa maendeleo ya taifa, licha ya kuwepo kwa changamoto katika kipindi
cha mpito.
Baba
Askofu Shao amesema hayo tarehe 15 Oktoba, 2017 wakati akihubiri katika
Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph,
Parokia ya Minaramiwili ambapo Mhe. Rais Magufuli ameungana na waumini
wa Kanisa Katoliki kusali Ibada ya Jumapili ya Dominika ya 28 ya mwaka A
wa Kanisa.
Akitoa
mfano wa nchi ya Zimbabwe ambayo Rais wake Mhe. Robert Mugabe aliamua
kuchukua hatua za kupigania maslahi ya Wazimbabwe na sasa wananchi wa
nchi hiyo wameanza kuzalisha bidhaa na kuziuza nje ya nchi, Askofu Shao
amesema hatua zinazochukuliwa na Mhe. Rais Magufuli kupambana na rushwa,
kupigania rasilimali za Watanzania, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji,
kukabiliana na wizi na ubadhilifu wa mali za umma na kubana matumizi,
zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.
“Hatutaweza
kusema tunaimaliza rushwa wakati tunaendelea kuishi kwa kupata fedha
ambazo hujazifanyia kazi, ni lazima tuishi machungu ya kuimaliza rushwa,
ni lazima tuishi machungu ya kuweka uadilifu katika utendaji wetu,
tusipoishi machungu hayo tutaishi dunia mbili, dunia ya rushwa na dunia
ya kujenga uchumi na uadilifu wa Watanzania, tukubali kujikatalia ili
tuweze kupata mazuri tuliyotaka” amesema Baba Askofu Shao.
Katika
salamu zake baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Mhe. Rais Magufuli
amemshukuru Baba Askofu Shao kwa mahubiri yake na ameungana nae
kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inachukua hatua za kupambana na
rushwa na kulinda rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi
wenyewe.
Mhe.
Rais Magufuli amesema hata Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage
Nyerere ambaye jana ametimiza miaka 18 tangu afariki dunia, alipiga vita
rushwa na alipigania rasilimali za nchi, hivyo ametaka Watanzania wote
kuungana katika juhudi hizo.
Mhe.
Dkt. Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli
amewashukuru Watanzania wote kwa maombi yao na amechangia Shilingi
Milioni 1 kwa ajili kwaya ya kanisa hilo na Shilingi Milioni 5 kwa ajili
ya maendeleo ya Kanisa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Zanzibar
15 Oktoba, 2017