NEC: Waliopoteza vitambulisho ruksa kupiga kura uchaguzi mdogo wa madiwani
Wapiga
kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga
kura katika uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43 unaotarajiwa
kufanyika Novemba 26, mwaka huu.
Hayo
yamesemwa jana Jumatatu Oktoba 16, 2017 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima mjini Dodoma ikiwa ni
siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na NEC.
Kailima
alisema wapiga kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia
vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), hati ya
kusafiria na leseni ya udereva.
“Tume
ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho kinasema mpiga kura
aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye kata
aliyojiandikisha, kwenye kituo alichopangiwa, kumridhisha msimamizi wa
kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye ndiye mpiga kura kwa
kumuonyesha kadi ya kupigia kura lakini kinasema kwamba Tume inaweza
ikaelekeza utambulisho mwingine wowote utakaomsaidia mpiga kura kuweza
kupiga kura iwapo kadi hana,” alisema Kailima.
Mkurugenzi
huyo wa uchaguzi alisema, “Tume kwa kuzingatia kifungu hicho, kuanzia
uchaguzi huu imetoa maelekezo kwenye mafunzo haya kwamba Tume imekubali
vitambulisho vifuatavyo vitumike, moja ni pasi ya kusafiria, pili ni
kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na Nida na mwisho ni leseni ya
udereva.”
Alisema
ruhusa hiyo imetolewa kwa sharti kwamba, “Majina na herufi yaliyopo
kwenye kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.”
Kailima
amesema NEC itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu
ya maagizo hayo, lakini akasisitiza kwamba tofauti yoyote itakayokuwepo
kwenye majina itamnyima mpiga kura fursa ya kupiga kura.
Alisema
uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa
mwaka 2015.