Mrisho Gambo: Sina Mpango wa Kugombea Ubunge Arusha

Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo amesema hana mpango wa kugombea ubunge jimbo la Arusha Mjini na anachofanya sasa ni kutekeleza ahadi za Rais John Magufuli kutatua kero za wananchi.

Akizungumza leo Jumamosi katika mkutano na waandishi wa habari Gambo amesema wanaosambaza uvumi kuwa atagombea ubunge Arusha ni wanasiasa ambao hawajiamini na wameshindwa kutatua kero za wananchi.

"Kazi ambazo nafanya kwa kushirikiana na wasaidizi wangu wakuu wa wilaya ni kutatua kero na tumeachana na mambo ya kisiasa kutembea na flashi wafanye wao sisi tunachapa kazi," amesema

Amesema ni ukweli uliowazi baadhi wabunge hawaonekani majimboni na hivyo kuwaachia viongozi wa Serikali kufanya kazi ambazo zilipaswa kufanywa na wabunge.

Akizungumzia tuhuma za kununuliwa madiwani wa Chadema ambazo zilitolewa na wabunge wa Chadema, Joshua Nassari na Godbless Lema, Gambo amesema anaamini hakuna masuala ya rushwa.

Gambo amesema madiwani ambao wamejiuzulu wameridhishwa na utendaji kazi mzuri wa Rais Magufuli.

 "Kuna madiwani wameondoka wa Arusha, Monduli, Ngorongoro, Arumeru, Hai, Iringa na maeneo mengine hawa wote wameridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano," amesema
Powered by Blogger.