Milioni 412 zatumika kumtibu Tundu Lissu
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe amesema gharama za matibabu ya Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi
nchini Kenya zimefikia Sh412.7 milioni.
Lissu
ambaye ni mwanasheria wa chama hicho, amelazwa hospitalini hapo tangu
Septemba 7 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa maeneo ya
nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Mbowe
akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Oktoba 17, 2017 jijini
Dar es Salaam, Tanzania amesema gharama ni kubwa, ila anawaomba
Watanzania wasichoke kuchangia kwa kuwa Lissu atarudi barabarani.
“Tunaishukuru
sana familia ya Lissu, imekuwa na msimamo kama Lissu mwenyewe.
Tumefanya kazi na familia na tutaendelea kufanya kazi na familia.
Tutakapokwenda katika matibabu ya tatu, tutaiacha kwa familia iwe
msemaji wa kwanza, mgonjwa anaweza kuongea na kujitambua,” amesema.
Kuhusu mchanganuo wa michango, Mbowe amesema wabunge wa Chadema wamechanga Sh48.4 milioni.
Amesema wananchi wamechangia Sh24.2 milioni kupitia simu ya Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko.
“Watu
mbalimbali wakiwemo wanachama wa Chadema wamechanga Sh90 milioni
kupitia akaunti iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB,” amesema.
Mbowe
amesema wabunge wote wakiwemo wa Chadema wamechanga Sh43 milioni na
kwamba, Watanzania walio nje ya nchi wamechanga kupitia Go fund me Dola
29,000 za Marekani.
Kiongozi huyo wa Chadema amemshukuru Mange Kimambi kwa kufanya kazi kubwa ya kuhamasisha michango.
Mbowe amesema wafanyabiashara wakihamasishwa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema wamechanga Dola 18,000.
Amesema wana orodha nzima ya wote waliochangia na amewaomba Watanzania waendelee kuwapigania.