Nassari Awajibu TAKUKURU......"Sitakaa Kimya"
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema kuwa hatokaa kimya endapo haoni hatua zinazochukuliwa.
Nassari amesema hayo leo Jumanne muda mchache baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola kumtaadharisha Nassari kuacha kugeuza taarifa anazoziwasilisha kwenye taasisi hiyo kuwa ni za kisiasa.
Hata
hivyo Nassari amesema, “Mlowola inabidi asome sheria ya ‘Whistle
blower’ ili nikae kimya lazima nione jitihada zinazofanyika kama hakuna
nitaendelea kuongea. Sitokubali kutishwa ili nisiendelee kupeleka
ushahidi ninachotaka kuona ni wahusika wanachukuliwa hatua sio madiwani,
wahusika wakuu ni mkuu wa wilaya na mkurugenzi,”
Awali
akizungumza leo Jumanne asubuhi, Mlowola ametoa tahadhari hiyo kwa
Nassari leo Jumanne, Oktoba 17, 2017 alipozungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam.
Amesema endapo Nassari ataendelea kuingiza siasa kwenye suala hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mlowola
amesema kitendo cha mwanasiasa huyo kuweka hadharani taarifa za
uchunguzi ni kinyume cha sheria kwa kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanyika
kwa siri na Mahakama ndiyo yenye jukumu la kuchukua hatua.
Amesema
Takukuru ina wajibu wa kumlinda mtoa taarifa lakini jukumu hilo
linakuwa tofauti kwa Nassari ambaye ameamua kujitokeza hadharani.
"Alicholeta
Nassari kwetu ni taarifa si ushahidi. Ameleta tumezipokea na
tunazifanyia kazi, inashangaza anapozungumza na vyombo vya habari na
kutuelekeza namna ya kufanya kazi," amesema.
Mlowola
amesema, "Tulishampa angalizo kuwa mambo tunayoongea ni siri lakini
mwenzetu inaonekana anafanya siasa kama anavyosema mwenyewe kuwa
ataendelea kuleta ushahidi kama series ya Isidingo."
Mkurugenzi
mkuu huyo amemtaka Nassari kuacha kukiingiza chombo hicho kwenye siasa
ili kifanye kazi kwa uhuru kama sheria inavyoelekeza.
"Nitoe
rai kwa Nassari na wengine wote, ukishaleta taarifa kwenye chombo
husika kama hiki kiache kifanye kazi. Hakuna sababu ya kukishinikiza au
kukiingiza kwenye malumbano ya kisiasa. Ukweli wa mambo utajulikana
mahakamani," amesema.