Makamu wa Rais awaonya Trafiki wanaogeuza tochi kuwa mtaji
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
amewaonya Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuacha kugeuza vifaa
vya kupimia mwendo wa magari maarufu kama tochi, kuwa chanzo cha wao
kujipatia rushwa.
Mama
Samia Suluhu ameyaeleza hayo jana wakati akifungua maadhimisho ya wiki
ya nenda kwa usalama ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro.
Makamu
wa Rais amewataka trafiki kujiepusha na vitendo vya rushwa na badala
yake watilie mkazo katika ulinzi wa usalama na usimamizi wa sheria za
barabarani.
Pia amewataka kutowanyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Samia
alieleza kuwa 76% ya ajali za barabarani huchangiwa na makosa ya
kibinadamu ikiwamo madereva kuendesha magari huku wakitumia simu zao,
uchovu unaosababisha madereva kusinzia, pamoja na kuendesha wakiwa
walevi.
Aliendelea
kwa kusema ubovu wa miundombinu ya barabara pamoja na ubovu wa magari
nayo imechangia kutokea kwa ajali za barabarani kwa asilimia 16.
Vile
vile alieleza kuwa kukosekana kwa umakini na uzembe wa madereva wa
bodaboda kumepelekea kuongezeka kwa idadi ya ajali za barabarani ambako
kungeweza kuepukika.
Samia amesema Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane.
“Mwaka
huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwa na ajali za pikipiki 42,721
zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597,” amesema.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeripotiwa kuwa na ajali 84 za bodaboda zilizosababisha vifo 61 na majeruhi 21.
Samia
ameeleza kusikitishwa kwa Tanzania kutajwa katika ripoti ya Shirika la
Afya Duniani (WHO) kuwa ni nchi inayoongoza kwa ajali ikiwa na asilimia
33.
Ameliagiza
Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kushirikiana na Jeshi la Polisi
Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau kuzingatia na kuelekeza nguvu
kwenye kudhibiti makosa makubwa matano hatarishi.
Makosa
yaliyotajwa ni pamoja na mwendo kasi, ulevi, kutovaa kofia ngumu,
kutovaa mikanda ya usalama katika gari na ukosefu wa vifaa vya usalama
kuwalinda watoto wadogo wakiwa ndani ya gari.