Lulu Michael Kizimbani Kesho Kutwa Kesi ya Steven Kanumba
Msanii
maarufu wa kike wa fani ya uigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael
Kimemeta, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya
aliyekuwa msanii maarufu wa kiume wa fani hiyo, Steven Kanumba,
keshokutwa atapanda kizimbani tena wakati kesi hiyo itakapoanza
kuunguruma.
Lulu
ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia,
kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu (PC), April 7, 2012,
nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican.
Kwa
mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam vya
mashauri ya jinai, kesi hiyo itasikilizwa keshokutwa na Jaji Sam
Rumanyika kuanzia keshokutwa, Alhamis Oktoba 19 hadi Jumatatu Oktoba 23,
mwaka huu.
Wakati
upande wa mashtaka (Jamhuri) ukidai kuwa Lulu alimuua Kanumba bila
kukusudia, hata hivyo Lulu mwenyewe wakati wa usikilizwaji wa awali
mahakamani ambapo alisomewa maelezo ya kesi hiyo alikana mashtaka hayo
ya kuua bila kukusudia.
Hivyo
kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa kuanzia keshokutwa, upande wa
mashtaka utakuwa na wajibu wa kuwaita mashahidi mahakamani kutoa
ushahidi na hata vielelezo kuthibitisha kuwa msanii huyo alitenda kosa
hilo.
Hata
hivyo ikiwa mara hii atakiri kosa hilo, basi Jamhuri haitalazimika
kuita mashahidi wake kuthibitisha kosa hilo bali mahakama itamtia
hatiani tu kwa kukiri kwake na kisha kumhukumu adhabu ambayo itaona kuwa
inafaa.
Mshtakiwa anayepatikana na hatia ya kosa la kuua bila kukusudia, adhabu ya juu huwa ni kifungo cha Maisha.
Kwa hiyo mahakama inaweza kumhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha, miaka 20, mitano, mwezi, siku, saa ama kumwachia huru kabisa.
Lulu
alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza April 10, 2012, katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kumuua Kanumba,
lakini hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka
ya kisheria kusikiliza kesi za namna hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Februari
17 msanii huyo alipandishwa kizimbani Mahakama Kuu na kujibu mashtaka
hayo kwa mara ya kwanza, wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo
(PH), ambapo alisomewa maelezo yote ya kesi inayomkabli.
Siku
hiyo Lulu alikubali kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba,
jambo ambalo ni miongoni mwa mambo manane ambayo aliyakiri mahakamani
hapo, kama mambo yasiyobishaniwa katika kesi hiyo, lakini akakana kumuua
Kanumba bila kukusudia.
Mambo
mengine ambayo Lulu aliyakiri mahakamani hapo yaliyoko katika maelezo
ya kesi hiyo ni pamoja na jina na anuani yake, kwenda nyumbani kwa
Kanumba usiku wa tukio hilo, kuwa na ugomvi na Kanumba pia Kanumba
kumzuia kutoka nje ya chumba alipojaribu kutoka ili akimbie.
Mengine
ni kufanikiwa kutoka nje ya chumba cha marehemu Kanumba, kumweleza
mdogo wa Kanumba (Seth Bosco) kuwa Kanumba ameanguka, kukamatwa kwake na
polisi eneo la Bamaga, saa 11 Alfajiri ya usiku wa tukio hilo na
kushtakiwa kwa kosa la kumuua Kanumba bila kukusudia.
Baada
ya Lulu kukana mashtaka, Wakili wa Serikali, Monica Mbogo aliiarifu
mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka
utakuwa na mashahidi wanne.
Aliwataja
mashahidi hao kuwa ni pamoja na Seth Bosco, Daktari binafsi aliyekuwa
akimhudumia Kanumba, Dk Paplas Kageiya, Ester Zephania na Askari D/Sgt
Ernatus wa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Pia
Wakili Mbogo aliwasilisha mahakamani vielelezo viwili vitakayotumika
kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo ambayo ni taarifa ya kitabibu
ya uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Kanumba na ramani ya eneo la tukio.
Lulu
kwa upande wake, mawakili wake Peter Kibatala na Fulgence Massawe
waliiarifu Mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwenye
utetezi watakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili. Hata hivyo
hawakutaja majina ya mashahidi hao.