Jafo aziagiza Halmashauri zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kurejesha mikopo yao
Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Selemani Jafo amezitaka Halmashauri zote zinazodaiwa na Bodi ya Mikopo
ya Serikali za Mitaa kurejesha madeni yao kabla ya Desemba 30 mwaka huu.
Jafo
ametoa agizo hilo jana Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari kuhusu marejesho ya mikopo katika bodi hiyo kutoka kwenye
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Bodi
ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani
ya shilingi bilioni 9.7 hadi Septemba 30, 2017 kwa Halmashauri 54. Hadi
Septemba 30, 2017 jumla ya shilingi 6.57 zilirejeshwa,” alisema Jafo.
Aliendelea
kwa kusema kuwa halmashauri nyingi zimejitahidi katika kurejesha mikopo
waliyochukua lakini kuna Halmashauri 9 zimeonyesha usugu uliopitiliza
katika kurejesha mikopo hiyo, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 2
hazijarejeshwa kutoka katika Halmashauri hizo.
Jafo
amezitaja Halmashauri zilizoonyesha usugu kuwa ni Halmashauri ya Jiji
la Mwanza na Mbeya, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Singida na
Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Karatu, Pangani, Igunga,
Mbinga, Mji Mbinga na Kongwa.
Aidha
amesema kuwa , kitendo cha usugu katika urejeshaji wa mikopo kinanyima
fursa kwa Halmashauri nyingine kupata mikopo kwa ajili ya kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hivyo
basi, Waziri Jafo amemtaka Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo kufanya
ufuatiliaji ili wadaiwa wote waweze kurejesha mikopo yao na wadaiwa sugu
kurejesha mikopo kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
Hata
hivyo Jafo ameitaka Bodi hiyo kuangalia utaratibu wa kupitisha mikopo
inayolenga ujenzi wa viwanda na uwekezaji katika Halmashauri ili kukuza
ajira na uchumi wa viwanda.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa
Richard Mfugale amesema kuwa bodi itatekeleza agizo la Waziri na tayari
imeshafanya mawasiliano na halmashauri zinazodaiwa kuona vyanzo vya
mapato watakavyoviachia kwa ajili ya kulipa madeni yao.
Bodi
ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ilianzishwa kwa lengo la kuziwezesha
Mamlaka za Serikali za Mitaa kupata mikopo ili kutekeleza miradi
mbalimbali ya kimaendeleo na utoaji huduma za jamii katika maeneo yao.