Dhahabu ya Mamilioni ya Pesa Yakamatwa Bandarini Ikitoroshwa

Mamlaka ya Bandari Tanzania, TPA, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imekamata madini ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu 6.2 yenye thamani ya Shilingi milioni 500 katika bandari ya Dar es salaam ndani ya gari aina ya Toyota Noah iliyokuwa na watu wawili.

Noah hiyo ilikuwa imewapeleka watu hao wawili bandarini na walipotaka kushuka, walishtukiwa na askari, lakini dereva alikimbia huku akiliacha gari eneo la tukio.

Watu hao walikuwa wakipeleka mzigo huo unaokisiwa kuwa na thamani ya Sh500.3 milioni visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema dhahabu hiyo iliyokamatwa katika eneo ambalo hutumiwa na wasafiri wanaokwenda Zanzibar ilikuwa katika miche mitano ambayo ilihifadhiwa kwenye begi.

Aliwataja watu hao kuwa ni Akifa Mohamed na Jaffer Hussein.

Kakoko alisema walipohojiwa, mmoja wao alidai kuwa nyaraka za dhahabu hiyo ziko Zanzibar, lakini uchunguzi wao umebaini hakuna nyaraka zozote.

Alisema mtuhumiwa mwingine alidai kuwa alikabidhiwa dhahabu hiyo ili aipeleke Zanzibar.

Kakoko alisema watuhumiwa wote wawili wako kituo cha Polisi cha Bandari ya Dar es Salaam na watafunguliwa shtaka la kupatikana na madini isivyo halali.

Akizungumzia walivyokamatwa, Kakoko alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 10, saa 5:20 usiku eneo la Azam Sea Link/DMI, wakati askari wa TPA na wa vyombo vya ulinzi na usalama, walipokuwa katika ukaguzi wa abiria, mizigo na magari yaliyokuwa yakiingia katika meli ya MV Azam Sea Link – I.

Alisema watu hao wawili walikuwa wa mwisho kufika eneo hilo wakiwa na gari hiyo aina ya Toyota Noah.

Alisema begi lililokuwa na dhahabu hiyo lilifichwa kwenye viti vya nyuma vya gari.

Alisema mwanzoni watuhumiwa hao walikataa kukaguliwa, lakini walipobanwa walikubali na ndipo walipoufuma mzigo huo.

Alisema gari hilo linashikiliwa na dereva anaendelea kusakwa.

“Tunaendelea kuimarisha ulinzi na usalama ili kudhibiti uhalifu kwa kufanya ukaguzi wa mizigo yote kabla ya kupakiwa melini,” alisema Kakoko.

Katika siku za karibuni Serikali katika vita yake ya kiuchumi imekuwa ikikamata watu tofauti wanaokutwa na madini na rasilimali nyingine za nchi.

Powered by Blogger.