Kwa Mara Ya Kwannza Katika Historia Wizara Ya Madini Kufanya Mnada Wa Tanzanite Mirerani
Wizara ya Madini kwa mara ya kwanza
itafanya mnada wa madini ya Tanzanite kutoka kampuni nne za uchimbaji na
biashara ya madini eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Kaimu Kamishna Msaidizi (Uchumi na Biashara ya Madini), Godleader Shoo amesema mnada huo utafanyika Oktoba 15.
Shoo
amesema utaratibu wa kufanya mnada huo ni jitihada za Serikali za
kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kuwasaidia
wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la
dunia.
Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini imemkariri Shoo akisema mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema atakayenunua madini hayo katika mnada ni atakayeshinda bei iliyowekwa.
Amezitaja
kampuni zitakazouza madini katika mnada huo kuwa ni TanzaniteOne,
Franone, Glitter Germs na Classic Gems. Amesema zitauza madini ghafi na
yaliyokatwa.
Shoo
amesema mnada utafanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wachimbaji,
wanunuzi, Shirika la Madini la Taifa (Stamico), vikosi vya ulinzi na
usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Wilaya ya
Simanjiro na Wizara ya Madini.
“Mnada
huu utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwa kuwa madini ya Tanzanite yana
thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi ili kujihadhari na watu wasio
waaminifu,” amesema Shoo.
Amesema
mnada utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi kwa uwazi ili
kuchangia pato la Taifa na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wauzaji,
wanunuzi na mali zao.
Shoo
amesema minada kama hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini
ya vito kama vile Zambia (emerald), Zimbabwe (almasi) na Afrika Kusini
(almasi).